Taught by
Stephen Armstrong
Taught by
Stephen ArmstrongUsiku wa leo tunamaliza somo letu la kuhusu juma la sabini la Danieli, Dhiki Kuu, na Vita vya Har–Magedoni vinavyohitimisha kipindi hiki cha uharibifu.
La muhimu zaidi, tunarudi tena kwenye matukio ya Kuja mara ya Pili kwa Yesu Kristo, kunakotokea kupitia mfululizo wa matukio mbalimbali.
Kwa hiyo, hebu turejee mandhari tuliyoiacha mwishoni mwa somo letu la juma lililopita.
Wayahudi wa mwisho wasioamini duniani wamejikusanya Yerusalemu chini ya shambulio linalofifia la Mpinga Kristo
Mpinga Kristo, ambaye anakaa ndani ya Shetani, ameazimia kumwangamiza kila Myahudi wa mwisho ili kuzuia kurudi kwa Kristo
Lakini adui tayari ameshindwa vita hivyo kwani siku chache kabla ya hapo Bwana alimwaga Roho Wake juu ya Israeli
Kwa sababu hiyo, taifa limemwamini Yesu, na Israeli yote imemwita Yesu kama alivyotaka kama sharti la kurudi Kwake.
Na sasa maneno ya Paulo yanatimizwa:
Paulo alikuwa akinukuu Isaya 59, ambayo inaelezea Kuja kwa Yesu Mara ya Pili kama jibu la Israeli kuja kwenye imani
Hapa kuna nukuu kamili:
Huo ndio wakati tumefikia… wakati Yesu anaweka miguu yake duniani tena ili kuanzisha Ufalme kwa ajili ya Israeli
Tulimwacha Yesu na watakatifu wa Kanisa na jeshi la malaika wakishuka duniani kujibu kilio cha Israeli
Nusu ya mji wa Yerusalemu tayari imechukuliwa, na wale waliobaki wamejaa hofu wakijua kwamba walimuua Masihi wao.
Bado hawajaelewa kwamba neema ya Mungu bado inakuja kuwaokoa
Wamekata tamaa na hawana tumaini hata wanapomlilia Mungu awahurumie
Ndiyo maana Zekaria alituambia wiki iliyopita kwamba mwitikio wa kwanza wa Israeli baada ya kumwamini Yesu ni kuomboleza
Hadithi ya Agano la Kale ya Yusufu na ndugu zake inatupa picha nzuri ya mabadiliko ya Israeli katikati ya majaribu na huzuni
Yusufu alikuwa mwana mpendwa wa Yakobo, jambo lililowafanya kaka zake wawaonee wivu
Yakobo alipomweka Yusufu kuwa mkuu wa ndugu zake, waliasi dhidi ya mamlaka yake na wakafanya njama dhidi yake
Na siku moja Yusufu alipofika kwa ndugu zake karibu na Dothani, waliamua kumuuza kwa wafanyabiashara wa Mataifa.
Sehemu hiyo ya hadithi ya Yusufu inaonyesha kuja kwa Yesu kwa mara ya kwanza alipowapa Israeli Ufalme ikiwa wangemruhusu awatawale.
Lakini kama ndugu zake Yusufu, ndugu zake Yesu walikataa utawala wake na badala yake wakamwuza Yesu mikononi mwa Warumi wa Mataifa
Baadaye, Yusufu anainuka kutawala juu ya mamlaka ya Mataifa, Misri, kama vile Yesu alivyofanyika Bwana juu ya Kanisa la Mataifa
Yusufu alikuwa wa pili katika usimamizi wa Misri, kama vile Mwana wa Mungu alivyo chini ya Baba Mungu
Baadaye, Bwana yuko tayari kuileta familia ya Yakobo chini ya utawala wa Yusufu, kwa hivyo analeta njaa nchini ili kumfanya Yakobo atafute msaada huko Misri.
Na siku moja ndugu zake Yusufu walifika mbele yake wakiwa na uhitaji mkubwa wa msaada.
Lakini Yusufu anaamua jinsi na wakati wa kujifunua kwa ndugu zake
Na wakati mwafaka ulipofika, Yusufu alifungua macho ya ndugu zake ili wamtambue
Wakati huu ni picha ya Kuja mara ya Pili kwa Kristo, na kwa Yusufu pamoja na Yesu jibu la kwanza la Wayahudi ni hofu
Angalia Yusufu analazimika kuwaambia ndugu zake wasimwogope, kwa sababu wanadhani atawatendea vibaya kwa dhambi yao
Lakini Yusufu anawaambia kwamba mpango huu wa Mungu ulikusudiwa kuleta ukombozi mkubwa kwao na kwa ulimwengu.
Na kwa kweli, kumkataa Yesu kwa Israeli wakati wa kuja kwake kwa mara ya kwanza kulikuwa sehemu ya mpango wa Mungu wa kuhakikisha kwamba ulimwengu mzima utabarikiwa mwishowe.
Na hicho ndicho tunachokiona sasa Yesu anaporudi duniani
Yuko karibu kuikabidhi Israeli Ufalme ulioahidiwa.
Lakini kwa sababu ya Israeli kumkataa Yesu hapo awali, Ufalme huo sasa utajumuisha jeshi kubwa la watakatifu wa Mataifa
Kama vile Yusufu alivyotawala si tu familia yake bali pia taifa zima la Misri
Basi sasa hebu turejee tena katika matukio ya hatua mbili za mwisho za vita vya Har–Magedoni, na hatua hizi mbili zinatokea katika maeneo mawili tofauti ya mapambano.
Kwanza, tunaona Mpinga Kristo akishambulia Yerusalemu, akiwa tayari ameharibu nusu ya mji
Na tuna mabaki ya Kiyahudi walioamini huko Botzrah wakishambuliwa pia kutoka kwa majeshi ya Mpinga Kristo yaliyotumwa kutoka Babeli.
Hawajafanikiwa kupata njia ya kuingia ngome hiyo lakini wanaendelea
Lakini vita vyote viwili vinakaribia kuisha, Yesu atakaporudi
Huenda umesikia wengine wakikuambia kwamba Kuja kwa Yesu Mara ya Pili kutatokea Yerusalemu
Na kwa hakika Yesu anakuja Yerusalemu - hatimaye, lakini Kuja Kwake kwa mara ya Pili hakuanzii hapo
Mahali pa kwanza pa kurudi Kwake si Yerusalemu…ni kwa wale Wayahudi waaminio katika ngome ya Botzrah
Tuanze na maelezo ya Isaya kuhusu Hatua ya IV ya vita…
Tazama mwanzoni mwa sura hii, Isaya anaelezea wakati katika historia ambapo majeshi yote ya mataifa yako tayari kuangamizwa na Bwana.
Na kwamba Bwana Mwenyewe ndiye atakayeleta mauaji haya dhidi ya mataifa
Mpinga Kristo ndiye kiongozi wa ulimwengu wote, wa mataifa yote, kwa hiyo jeshi lake ni jeshi la mataifa yote
Na katika mstari wa 4 tunaona vita hivi vikitokea sambamba na wakati ambapo mbingu zitachakaa na kutoweka, jambo linalozungumzia kipindi cha Dhiki Kuu.
Anga imekunjwa kama hati (au gombo la kitabu) na mimea yote imetoweka
Ni wazi kwamba maelezo haya yanafanana sana na yale tuliyoyaona wakati wa Dhiki Kuu
Kwa hiyo vita hivi vya majeshi ya mataifa dhidi ya Bwana vimewekwa katika wakati wa Dhiki, kulingana na Isaya
Kisha katika mstari wa 5-6, Bwana Mwenyewe anaanza kuzungumza kuhusu vita
Upanga wa Bwana umeshiba Mbinguni, na neno kushiba linamaanisha kuridhika (kutosheka kikamilifu), au kushiba (kujazwa).
Kwa hiyo, upanga wa Bwana umepokea utimilifu wake kutoka mbinguni, jambo linaloashiria kwamba sasa uko tayari kupigana kwa namna mpya.
Ndiyo maana katika mstari wa 5 Bwana anasema kwamba upanga Wake utashuka kwa ajili ya hukumu.
Marejeleo ya kushuka ni muhimu, kwa sababu yanaonyesha kwamba kuna mabadiliko yanayotokea katika mstari huo.
Upanga huo unatoka mbinguni na kuja duniani, jambo linaloashiria Kuja kwa Mara ya Pili kwa Kristo.
Na Isaya anasema kwamba uharibifu wa mataifa yote utakuja mikononi mwa Mungu kuanzia Edomu, hasa Botzrah
Isaya anasema Bwana ameandaa dhabihu katika Edomu, huko Botzrah
Na pia ona kwamba katika mstari wa 3, miili ya waliouawa itaonekana juu ya mlima ambao utatiwa doa na damu yao.
Hili ni rejeo la wazi kwa safu ya milima inayozunguka eneo la wazi la Botsra, au Petra ya kisasa.
Maelezo haya yanathibitisha kwamba Bwana atalinda kambi ya watu wake huko Petra na kuwaangamiza wote wanaoishambulia.
Uharibifu huu hutokea wakati wa Dhiki na sambamba na kushuka kwa Bwana kutoka Mbinguni, ambako ni mwishoni mwa Dhiki.
Shambulio la Yesu huko Botzrah ni Hatua ya IV ya Vita vya Har-Magedoni, wakati Bwana atakapoharibu majeshi ya Mpinga Kristo huko
Bwana peke Yake ndiye anayepigana vita hivyo, na maandiko hayataji mtu mwingine wala kiumbe kingine chochote kinachoshiriki mapambano hayo—ni Bwana peke Yake.
Kwa hiyo Bwana anashuka kama ilivyoelezwa katika Ufunuo 19 akiwa na majeshi nyuma yake, na anapofika Petra anaangamiza majeshi ya Mpinga Kristo.
Sasa Mika anatuambia kile ambacho Yesu atafanya baadaye
Tulisoma Mika 2:12 hapo awali tulipokuwa tukijifunza kuhusu kukimbia kwa Israeli kwenda jangwani katika Ufunuo 12.
Mika ndiye nabii anayetaja mahali pa ulinzi wa Israeli: Botzrah
Katika Kiebrania, maneno yaliyotafsiriwa kuwa “zizini” au “kundini” ni neno Botsra, ambalo linaelezea asili ya mahali hapo kama eneo la ulinzi na usalama.
Ni neno halisi la Kiebrania linalomaanisha zizi la kondoo na pia ni jina sahihi la mji wa Petra wa leo.
Hapa ndipo mahali ambapo mabaki wa Israeli waaminio watahifadhiwa salama kwa nusu ya pili ya Dhiki
Na sasa kwa kuwa Dhiki inaisha na Yesu amerudi, ni wakati wa kuwaacha "kondoo" kutoka katika "zizi" hilo
Na katika mstari unaofuata Mika anaelezea kuachiliwa huko siku ile Yesu atakapokuja
Mika anasema kwamba “Mvunja-njia” au “Mkombozi” atakwenda mbele ya wale waliokuwa wamehifadhiwa mahali hapo.
“Mvunja-njia” huyo ni rejeo kwa Yule anayewaweka huru, akivunja vizuizi na kuwatoa kutoka mahali hapo.
Neno la Kiebrania lililotafsiriwa kuwa “mvunja-njia” linamaanisha mtu anayebomoa, anayefungua njia, au anayevunja uzio unaozuia.
Huyu ndiye Bwana Mwenyewe, na angalia kwamba wanamfuata nje wakipitia lango na kutoka nje kupitia hilo
Kupitia lango ni picha nyingine ya zizi la kondoo na jinsi mchungaji anavyowatoa kondoo wake kwenda malishoni.
Huu ni msafara mtulivu na wa amani kama kondoo wanaomfuata mchungaji wao kwa utulivu anapowaongoza nje
Mika anaongeza kwamba mfalme wao anawatangulia mbele yao, na Bwana yuko akiwaongoza.
Kwa hiyo, hii ni picha ya mabaki ya Israeli yakitolewa kutoka mahali pao pa ulinzi na matunzo mwishoni mwa Dhiki Kuu.
Yesu anawashinda wale wanaowashambulia mabaki na kisha anafungua lango na kuwaongoza nje
Hatujui hili litakuwa lango la aina gani, lakini tunaweza kulinganisha hali hiyo na safina ya Nuhu.
Safina ilikuwa na mlango ambao Mungu aliufunga kabla ya gharika na kuufungua baada ya safina kutua salama, na ndivyo itakavyokuwa hapa.
Kwa hiyo, Yesu anapowaweka huru Wayahudi hawa waaminio kutoka Petra, tunaweza kufikiria tukio linalofanana na Kutoka kwa Waisraeli kutoka Misri.
Kama Musa alivyoongoza watu wa Israeli kupitia jangwa la Sinai, sasa Yesu anawaongoza watu Wake katika jangwa la wazi.
Tofauti ni kwamba sasa Yesu ndiye Kiongozi wao wa moja kwa moja. ndiyo kusema kwamba ni sasa tu Yesu anachukua nafasi kama ile aliyochezwa na Charlton Heston, mwigizaji maarufu wa Marekani aliyeigiza Musa katika filamu ya The Ten Commandments.Ni sasa tu Yesu, anachukua nafasi ya Charlton Heston
Lakini Bwana anapowaongoza kutoka huko, wanaelekea wapi?
Isaya anatupa jibu
Ili kuelewa maandiko haya vizuri, ni lazima tuelewe muktadha wake.
Isaya anaandika kwa mtazamo wa mtu wa kwanza akiwa amesimama juu ya kuta za Yerusalemu wakati wa shambulio la Mpinga Kristo dhidi ya mji huo.
Huo ndio muktadha wa sura hii. Kwa hiyo fikiria nabii akiwa juu ya ukuta unaobomoka, mji ukishambuliwa, moshi ukifuka kila mahali.
Kuna vurugu kila upande, mapigano yanaendelea mitaani, na majeshi yameuzunguka mji kando ya kuta zake.
Katikati ya hali hiyo, nabii yuko juu ya ukuta akitazama upande wa mashariki kuelekea Mlima wa Mizeituni.
Na anapotazama kwa mbali, anaanza kuuliza maswali
Anauliza, “Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu? Amevaa mavazi ya fahari na utukufu.”
Unakumbuka jinsi Yohana alivyoelezea kuonekana kwa Yesu wakati wa Kuja Kwake Mara ya Pili?
Yesu anarudi katika utukufu Wake, na maelezo ya Isaya kuhusu Yesu akiwa katika utukufu, mwenye rangi zinazong'aa na ghadhabu kali, yanafanana na maelezo ya Yohana.
Amevaa vazi lililochovywa katika damu, na kama nilivyotaja wiki iliyopita, damu hiyo ilikuwa ishara ya vita ambavyo angeenda kupigana.
Na sasa Isaya anatuambia kwamba damu inatoka katika vita vya Botzrah
Isaya anasema kwamba mavazi Yake yamekuwa mekundu kwa sababu ya kukanyaga shinikizo la divai (winepress), jambo linaloashiria ghadhabu kali ya hukumu ya Mungu.
Kwa hiyo Isaya anamwona Bwana akija Yerusalemu kutoka Botzra akiwa na vazi lake lililojaa damu kutokana na vita
Lakini Isaya haelewi kwa nini Bwana ameonekana kwa njia hii, hivyo anauliza maelezo kuhusu jambo hilo.
Bwana anaelezea kwamba alipigana vita hiyo peke yake
Anasema aliwakanyaga mataifa, akielezea vita alivyokutana navyo huko Bosra.
Anasema alikanyaga shinikizo la divai peke yake, akimaanisha kumwaga ghadhabu ya Bwana dhidi ya majeshi huko Botzrah
Aliwakanyaga kwa hasira ya Mungu na damu yao ikachafua mavazi yake kwa sababu siku ya ukombozi na kisasi ilikuwa imefika.
Ona kwamba Bwana anasema alipigana vita hivi peke yake, na hakuna aliyemsaidia.
Alishangazwa sana—yaani, alisikitishwa sana na kushtushwa—na kile alichokiona huko Botzrah
Kisha, kwa mamlaka na uwezo wake binafsi, akachukua hatua ya kuliangamiza jeshi lile dhaifu na la kusikitisha lililokuwa likimngojea.
Lugha kali iliyotumiwa hapa inaonyesha hasira kuu ya Mungu dhidi ya uovu na kutomcha Mungu kwa ulimwengu atakavyoukuta wakati wa kurudi kwake
Kumbuka maneno ya Bwana alipokuja mara ya kwanza:
Bwana alitabiri kwamba atakaporudi, hatakuta dunia iliyojawa na imani ikimngoja.
Badala yake, kurudi Kwake kutakabiliwa na ulimwengu uliojaa kutokuamini kwa kiwango kikubwa, usiotubu, na wenye chuki dhidi ya Mungu na watu Wake.
Kwa hiyo, Isaya anamwona Bwana akija Yerusalemu akiongoza msafara wa mabaki ya waaminifu wanaoandamana pamoja na Kristo.
Inavutia kufikiria jinsi kundi hili linavyoweza kusafiri umbali huo kwa muda mfupi, kwa kuwa ni takriban maili 75 (kilomita 120) kwa njia ya moja kwa moja (yaani, kama ndege arukavyo).
Je, wanasafiri kwa njia ya kawaida au kwa uwezo wa kimuujiza?
Ni wazi kwamba Yesu Mwenyewe ana uwezo wa kufika mahali popote bila kizuizi, na majeshi Yake yanaweza kwenda popote anapokwenda.
Kwa hiyo, inawezekana kwamba Yesu anawahamisha mabaki hayo kwa njia ya kimuujiza ili wafike Yerusalemu kwa haraka.
Sasa Kristo anakaribia mji wa Yerusalemu, na anapofanya hivyo, anakutana na mstari wa pili wa mbele wa vita (au sehemu ya pili ya vita) vya Har–Magedoni.
Na kama ilivyokuwa katika sehemu ya kwanza ya vita, tunaona jeshi lisilo na mpangilio mzuri la Mpinga Kristo likijaribu kwa nguvu zote kuingia ndani ya mji.
Bwana amekuwa akiulinda mji huo, akiwatia nguvu raia wake kwa njia ya kimuujiza ili waweze kupambana na wavamizi.
Ingawa wamefanya uharibifu fulani, bado kuna upinzani unaoendelea
Lakini hawawezi kuendelea kwa muda mrefu zaidi... Ndipo Yesu na majeshi Yake wanapotokea.
Katika Zekaria 14 tunaona jinsi vita vinavyoendelea Yesu anapowasili Yerusalemu hatua kwa hatua
Tutajifunza vita hivi vya mwisho vya enzi yetu kwa hatua kadhaa kama Zekaria anavyovielezea
Kuanzia na Yesu akikaribia mji
Hapo awali, tulisoma mstari wa 1-2 wa sura hii tulipojifunza Hatua ya III ya Vita vya Har–Magedoni, shambulio la kwanza dhidi ya Yerusalemu
Unakumbuka kwamba Mpinga Kristo alihama kutoka kaskazini mwa Israeli kuelekea kusini kisha akapanda kutoka magharibi ili kuzingira Yerusalemu
Vita vinapoanza, Mpinga Kristo anaanza kupanda kuta na kuingia mjini
Zekaria anasema kwamba mji unavamiwa, nusu ya wakazi wa mji wanachukuliwa mateka na huenda wengi wao wakauawa.
Wanawake wanabakwa na inawezekana wengi wao pia wanauawa.
Na Hosea alituambia kwamba vita vingeendelea kwa siku 2, na kisha siku ya tatu taifa la Israeli lingeletwa kwenye imani na Roho wa Mungu.
Na wanapoitikia kwa kumwita Yesu, Yeye huwajia kuwaokoa.
Hasa anawajia kutoka Botzrah, akiongoza kundi la Wayahudi waaminio waliokuwa wakimngojea huko.
Zekaria anaanza simulizi hiyo katika mstari wa 3, akielezea kwamba Bwana anakuja kupigania Yerusalemu
Bwana anapigana na mataifa hayo yanayokuja dhidi ya mji
Na katika mstari wa 4 tunaambiwa miguu ya Bwana imesimama juu ya Mlima wa Mizeituni
Wakati mwingine kifungu hicho hufasiriwa vibaya kana kwamba Yesu alitua moja kwa moja juu ya Mlima wa Mizeituni, lakini Zekaria hasemi hivyo.
Anasema tu kwamba Yesu alisimama hapo, na Isaya anatueleza kwamba alifika hapo akitokea Bosra.
Kwa hiyo Yesu anafika kwenye safu ya milima mashariki mwa Yerusalemu na kusimama, akisimama moja kwa moja juu ya Mlima wa Mizeituni
Kutoka hapo anaweza kuutazama chini ndani ya mji na kushuhudia shambulio la Mpinga Kristo.
Na ni kutoka hapa ndipo Yesu anaanza kuulinda mji
Hii ni Hatua ya Tano ya Vita vya Har-Magedoni, vita vya mwisho kabisa vya Enzi hii.
Lakini Bwana hashuki kwa kasi mlimani na kuingia mjini kupigana uso kwa uso na askari.
Badala yake, Bwana anaanza vita kwa mbali, kwa kubadilisha mandhari ya eneo la vita
Ona kwamba Yesu anaikaribia Yerusalemu kutoka mashariki, jambo linaloendana na ukweli kwamba anatoka Bosra.
Na pia tunakumbuka majeshi ya Mpinga Kristo yanashambulia kutoka magharibi, kulingana na Danieli 12
Kwa hiyo Yesu anapowasili, Yeye yuko mashariki, Mpinga Kristo yuko magharibi, na mabaki ya Yerusalemu yako katikati yao.
Na Zekaria anasema kwamba Yesu anaposimama juu ya Mlima wa Mizeituni, anaamuru mlima upasuke vipande viwili, mashariki hadi magharibi
Kisha sehemu hizo mbili za mlima zitatengana, nusu moja kuelekea kaskazini na nusu nyingine kuelekea kusini.
Hali hii itaunda mfereji au bonde linaloelekea mashariki kutoka mjini
Kumbuka kwamba katika mtazamo huu wa kinabii, milima mingi ya dunia tayari imeondolewa na mabadiliko makubwa ya kijiografia yaliyotangulia, isipokuwa mlima ambao Yerusalemu umejengwa juu yake pamoja na safu ya milima inayouzunguka.
Kwa hiyo mlima wenyewe unapopasuliwa, huunda njia inayotoa ulinzi kamili kwa wale walio ndani yake.
Kisha Zekaria anasema kwamba Wayahudi walioko Yerusalemu watakimbia (watatoroka) vita kupitia kwenye njia hiyo
Kwa sababu shambulio linakuja kutoka magharibi, njia ya kutokea itakuwa kuelekea mashariki kupitia bonde hili.
Katika mstari wa 5, Zekaria anasema kwamba Wayahudi watakimbia kupitia bonde ambalo Bwana ameunda ardhini.
Je, jambo hili linakukumbusha wakati mwingine ambapo Bwana aliwaokoa Waisraeli waliokuwa wakikimbia kutoka kwa jeshi lililokuwa likiwafuatilia liwashambulie kwa kuunda au kutengeneza bonde la ulinzi?
Tunakumbuka Israeli wakimkimbia Farao kupitia bonde la maji lililoundwa katika Bahari Nyekundu (bahari ya Shamu), safari nyingine kutoka Magharibi hadi Mashariki.
Hatimaye, Zekaria anasema Bwana ataingia mjini akiwa pamoja na watakatifu wake wote nyuma yake ili kumalizia vita hiyo
Ni baada tu ya wasio na hatia kuondolewa kwenye hatari ndipo Bwana anasonga mbele kuanzisha shambulio lake la mwisho.
Habakuki anatupa mtazamo mwingine wa harakati hii kutoka Petra hadi Yerusalemu
Kifungu hiki ni maelezo ya Kurudi kwa Bwana Mara ya Pili Yerusalemu, na angalia kinaanza na marejeo ya kijiografia
Nabii anasema Bwana anakuja Yerusalemu kutoka Temani au Mlima Parani.
Haya ni majina ya kale ya Edomu, ambapo tunapata Botzrah
Na Bwana anafika akiwa na mng’ao kama mwanga wa jua, jambo linalothibitisha maelezo mengine tuliyosoma kuhusu kuja Kwake kwa mara ya pili.
Katika mstari wa 6, Habakuki anaelezea uharibifu wa kidunia uliotangulia kurudi Kwake
Tauni, magonjwa, milima ikitikisika, n.k.
Haya ni marejeo ya matukio ya Dhiki Kuu yanayotangulia kurudi kwa Yesu.
Ghadhabu yake ilikuwa dhidi ya bahari, mito, na jua na mwezi vilisimama mahali pake kisha vikatoweka kwa mwanga wa kuonekana kwake.
Maelezo haya yote yanaonyesha matukio halisi yanayolingana na yale tuliyojifunza katika sehemu nyingine.
Kwa hiyo tunajua nabii huyu anazungumzia tukio lilelile—kuja kwa mara ya pili kwa Bwana mwishoni mwa kipindi cha Dhiki Kuu.
Lakini katika Habakuki, katika mstari wa 8 anauliza kwa njia ya swali la balagha kama ghadhabu ya Mungu ilikuwa imeelekezwa dhidi ya mito, milima na bahari zenyewe?
Kwa maneno mengine, je, Bwana alikuwa ameghadhibika na Uumbaji wenyewe?
Katika mstari wa 12-13 nabii anajibu hapana… Bwana hakuwa na hasira dhidi ya uumbaji wenyewe
Badala yake, Habakuki anasema kwamba alikuwa akikasirika dhidi ya majeshi na mataifa ya dunia.
Kwa hiyo baada ya Wayahudi kutoroka, Yesu anaingia mjini kutoka mashariki, na kukutana na Mpinga Kristo huku yeye na majeshi yake wakisonga mbele kutoka magharibi.
Anapigana kwa ajili ya wokovu wa watu wake, Israeli, na mwishoni mwa mstari wa 13, anasema Bwana atakipiga kichwa cha nyumba ya uovu.
Kichwa cha nyumba ya uovu ni marejeo dhahiri kwa Mpinga Kristo ambaye ndiye kichwa cha ulimwengu na yote yaliyo maovu.
Pigo la Bwana linamkata kutoka paja hadi shingo—ambalo ni maelezo ya picha, kina na kutisha ya kifo cha Mpinga Kristo.
Amepasuliwa na kuchanuliwa ngozi, amekatwakatwa kwa upanga wa Kristo
Kwa hiyo wakati Yesu anapofika Yerusalemu, shambulio lake linasababisha kifo cha Mpinga Kristo pamoja na majeshi yake yote.
Tunaona uthibitisho wa matokeo haya katika 2 Wathesalonike
Kuonekana kwa Bwana kutasababisha mwisho wa Mpinga Kristo na mwisho wake utakuja kwa kutokana na pumzi ya kinywa cha Kristo.
Kumbuka, neno (au pumzi) la Kristo linaitwa upanga katika Maandiko
Kwa hiyo Yesu anapigana kihalisi na neno Lake pekee, kwa sababu neno la Bwana ni nguvu yake yenyewe, nguvu pekee ya kweli katika Ulimwengu.
Wraka wa Waebrania pia unasema kwamba neno la Mungu ni gundi inayoshikilia Ulimwengu pamoja
Kwa hiyo neno la Yesu linatosha zaidi kuharibu chochote, kwa sababu ndilo kitu pekee kinachoshikilia kila kitu pamoja.
Kwa hiyo kwa neno la Kristo, mwili wa Mpinga Kristo unapasuliwa, majeshi yake yanakufa kwa namna inayofanana, na vita inaisha haraka.
Kumbuka kitabu cha Ufunuo sura ya 14 kilitupa hakikisho la uharibifu huo
Huu ndio wakati wa umwagaji damu huku Yesu akimaliza maisha ya maelfu na labda mamilioni ya wanadamu kwa papo hapo
Kifo chao ni cha ghafla na cha kikatili kiasi kwamba damu yao yote inamwagika mara moja, ikijaza Bonde la Kidron na kutiririka hadi umbali wa maili 200.
Sasa kilichobaki ni kusafisha machafuko hayo, na ni machafuko makubwa kweli, lakini Bwana ana mpango wake.
Sasa tumerudi kwenye mtazamo wa mbinguni wa Yohana kuhusu matukio hayo
Kumbuka, tunajifunza kurudi kwa Kristo kutoka pande mbili: mtazamo wa duniani na mtazamo wa mbinguni.
Manabii wa Agano la Kale wanatupa mtazamo kutoka duniani, iwe ni Botzrah au Yerusalemu
Wakati Yohana anaona matukio kutoka mahali pake pa kuona Mbinguni, ambapo pia ndipo tutashuhudia mambo haya kwa shukrani
Tayari tulianza na mtazamo wa Yohana mwanzoni mwa sura hii, na kisha tukajifunza mtazamo wa kidunia
Sasa Yesu na msafara wake wamefika duniani, kwa hiyo katika hatua hii mitazamo miwili inaungana
Habakuki alieleza mwisho wa vurugu huko Yerusalemu ukiwa na maiti nyingi, na sasa Yohana anaona tukio lilelile kwa njia yake.
Ni kana kwamba Yohana hakuwahi hakuona vita yenyewe, bali anafika baada ya vita kumalizika na anaona uharibifu uliosalia.
Baada ya vita kuisha, ulimwengu wa malaika wa Yesu unaanza kazi ya kuita kikosi cha kusafisha
Malaika Mbinguni anawaita ndege walio katikati ya mbingu waje wakusanyike kwa ajili ya mlo mzuri
Neno katikati ya Mbingu kwa kawaida ni neno la Kibiblia linalomaanisha anga za nje au hata za juu
Lakini hawa ni ndege wanaokula nyama, kama tai, kwa hiyo katika muktadha huu neno katikati ya Mbingu linaeleweka kwa njia tofauti.
Katika Kigiriki inaweza pia kutafsiriwa zenith, kama vile katika sehemu ya juu zaidi angani, ambayo ndiyo maana iliyokusudiwa hapa
Ezekieli pia anaonyesha kwamba Mungu wakati mwingine hutumia ndege na wanyama kula maiti za waliokufa (Ezekieli 29), kama ishara ya hukumu.
Na hivyo Hatua ya Tano ya Vita vya Har–Magedoni, Enzi ya Mataifa, na Dhiki inafikia mwisho…dunia imepumzika kutokana na vita
Majeshi yote yanayopinga yanashindwa, na Waisraeli wote duniani waliokusudiwa kuokolewa wanaokolewa.
Siku zote kuna Mataifa waaminio duniani wakati wa kuja kwa Yesu
Na kuna Mataifa wasioamini ambao hawakuwa sehemu ya jeshi la vita na hivyo hawakuangamizwa katika mapigano ya mwisho.
Hatimaye, tutachunguza kinachotokea kwa makundi haya baada ya kurudi kwa Kristo katika somo linalofuata.
Lakini kabla ya hapo, tunahitaji kuona hatima ya wale waliochochea uasi wa dunia: wahusika wa “utatu wa uongo.”
Katika mstari wa 20 tunasoma kuhusu kuangamizwa na mwisho wa mnyama au Mpinga Kristo na nabii wa uongo.
Wote wawili wanapewa hatima ya kipekee ya kutupwa wakiwa hai katika Ziwa la Moto.
Lakini kama tulivyoona kwingineko, kuna mengi zaidi yanayoendelea hapa kuliko Yohana alivyoandika katika muhtasari huu mfupi katika Ufunuo.
Kwanza, Mpinga Kristo na nabii wa uongo ni wanadamu, bila shaka
Lakini wakati wa nusu ya pili ya Dhiki, wote wawili ni vyombo vya Shetani
Tunajua Mpinga Kristo anakaa ndani ya Shetani, na nabii wa uongo huenda akawa chini ya nguvu ya pepo mkuu.
Wakati mwili unapokufa, roho zilizokuwa ndani yake hutoka, kama vile roho ya mtu inavyotoka wakati wa kifo.
Kwa kuwa tunajua kwamba Mpinga Kristo aliuawa wakati Yesu aliporudi, kama Habakuki na Paulo wanavyotuonyesha,
Na pengine, nabii wa uongo pia anakufa vitani
Kisha tunaweza kudhani kwamba Shetani na mapepo yake waliachiliwa, na roho za wanadamu wenyewe pia ziliachiliwa kutoka kwenye miili yao.
Kwa hiyo nini kitatokea kwa kila mmoja wa wahusika hawa? Kwanza, roho ya Mpinga Kristo inashuka kwa muda mfupi kuzimu
Isaya anatoa maelezo marefu ya kile kinachotokea kwa roho ya Mpinga Kristo inapofika Kuzimu
Katika Isaya, tukio hili litatokea wakati taifa la Israeli litakapokuwa limekwisha kurejeshwa, nabii anasema:
Bwana atawachukua watu wake, akiwa amewahurumia, na kuwaweka katika nchi yao.
Watawaleta watu wengine (Mataifa) pamoja nao katika Ufalme
Na Bwana atawapa Israeli pumziko kutoka katika maumivu na misukosuko yao.
Ni wazi kwamba hiyo ni rejea ya Israeli kuingia katika Ufalme
Hivyo huo ndio muktadha wetu, na katika wakati huo, tunamsikia Israeli akimdhihaki Mfalme wa Babeli.
Kumbuka, Babeli ni neno la Biblia linalomaanisha Ufalme wa Shetani na yote unayowakilisha
Na mfalme huyu wa Babeli aliwahi kutawala watu kwa mapigo yasiyokoma na kuyashinda mataifa
Kwa hiyo katika muktadha huu, hii ni rejea ya Mpinga Kristo.
Lakini sasa dunia imepumzika na mfalme huyu anajikuta katika Sheol au Kuzimu (mstari wa 11, mst. 15), akipumzika kwenye kitanda cha funza
Angalia katika mstari wa 19, alikuwa amevikwa mavazi ya waliouawa, marejeo ya ufufuo wake katikati ya Dhiki Kuu.
Kisha katika mstari wa 20 tunaambiwa kwamba hataunganishwa na watu wake katika maziko.
Watu wake ni mataifa yaliyomfuata na kwenda kwenye mauti yao hadi kuzimu wakati wa Kuja kwa Yesu Mara ya Pili
Lakini Mpinga Kristo hatajiunga nao, kwa sababu atatolewa kutoka kuzimu karibu mara moja (upesi).
Na kama Yohana anavyotuambia, atapelekwa moja kwa moja katika Ziwa la Moto pamoja na Nabii wa Uongo.
Kwa hiyo Mpinga Kristo na nabii wa uongo wanakufa katika vita vya mwisho, na wanapokufa wanaingia Jehanamu kama roho zote lakini kwa muda mfupi tu.
Ni muda mfupi tu wa kutosha kwao kukutana na kukaribishwa na wafalme wa dunia waliowatangulia katika mahali hapo pa kutisha.
Angalia katika Isaya 14 wanamdhihaki Mpinga Kristo kwa kushushwa chini sana
Huu ndio upokezi ambao makafiri (waovu) wote wakubwa na wenye nguvu hupokea wanapokufa na kuingia Jehanamu.
Wanazungukwa na watu wa aina yao ambao kama wao wanateseka.
Na bado wana kumbukumbu za kila mmoja na maisha waliyoyaacha nyuma
Kwa hiyo Mpinga Kristo anafufuliwa upesi (mara moja) katika mwili mpya wa milele na kisha kutupwa katika makao ya kudumu kwa wasioamini.
Yeye na nabii wa uongo wanaingia katika Ziwa la Moto wakiwa hai, na ndivyo wasioamini wote watakavyoingia katika eneo hilo.
Wanadamu wote hufufuliwa katika miili mipya, waamini na wasioamini
Tofauti ni mahali ambapo makundi hayo mawili yatatumia umilele wao.
Tofauti ya Mpinga Kristo ya kuwa wa kwanza kufufuliwa na kutupwa katika Ziwa la Moto ni mgeuko wa kejeli katika hadithi yetu.
Shetani, Mpinga Kristo na nabii wa uongo walipokutana, walijaribu kuunda utatu bandia na wa uongo.
Walikuwa wakiiga Utatu wa kweli wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu
Na bila kukusudia, wanaakisi huo uongo hata katika kifo chao.
Kristo ndiye matunda ya kwanza ya ufufuo wa uzima wa milele
Maana yake alikuwa mwanadamu wa kwanza kufufuliwa katika mwili wa milele ambao haufi kamwe
Vivyo hivyo, Mpinga Kristo atakuwa matunda ya kwanza ya ufufuo miongoni mwa wale watakaoingia katika kifo cha milele.
Wiki ijayo tutaingia katika Sura ya 20 ambayo inaelezea kipindi cha Ufalme, lakini hatutaingia sana katika Sura hiyo mara moja.
Kwa sababu kwanza tunaingia katika kipindi kisichojulikana sana cha ratiba ya Mungu kinachoitwa kipindi cha siku 75
Tutaanzisha dhana hiyo wiki ijayo na kuelezea madhumuni yake
Mara tutakapomaliza kipindi hicho, tutaingia katika utangulizi wa kipindi cha Ufalme wa Milenia na na uchunguzi mpana wa kipindi hicho.