Taught by
Stephen Armstrong
Taught by
Stephen ArmstrongUsiku wa leo ni Sehemu ya 2 ya somo letu la Ufalme
Tunaendelea kusoma kuhusu kipindi hiki cha kuvutia kwa kugawa somo letu katika sehemu (vipengele) kadhaa.
Wiki iliyopita tuliangalia mabadiliko ya Uumbaji, ardhi, wanyama na serikali
Hebu tufupishe tulichojifunza katika maeneo hayo
Kwanza, ulimwengu wa asili utaanza kurudi katika hali ambayo iliijua kabla ya anguko la Adamu
Ufalme wa wanyama hautaendelea tena kuwa na uhusiano wa wanyama walao wengine na wale wanaoliwa.
Vivyo hivyo, wanadamu hawatakuwa tena katika hatari ya kushambuliwa na wanyama.
Na mabadiliko haya yanawakilisha kugeuzwa kwa sehemu kwa laana ambazo Mungu alizitangaza juu ya dunia baada ya anguko.
Hata hivyo, badiliko moja halijageuzwa: nyoka bado anatambaa ardhini
Ukumbusho huu wa udanganyifu wa Shetani unabaki duniani kwa sababu adui mwenyewe bado yupo kwa muda
Kisha tulijifunza kwamba Israeli itarudi katika nchi yake, na mipaka yake itapanuliwa sana kuliko mipaka ya sasa.
Itakuwa karibu na mipaka ya siku za Sulemani
Na Israeli itakuwa taifa kuu duniani kwa sababu Yesu mwenyewe ataishi Yerusalemu
Miongoni mwa mabadiliko mengine ya asili ni kuonekana kwa maumbo na miundo mipya ya ardhi katika Israeli, kuanzia na ardhi ambayo itazaa mazao mengi bila juhudi kubwa.
Hilo pia ni kinyume cha laana iliyoikumba nchi
Na milima itakuwa na vijito juu, ili maji yawe kila mahali na ardhi iwe rahisi kulimwa
Mlima unaoshikilia hekalu utakuwa mlima mkuu siku hiyo
Na kutoka kwenye hekalu, kutatiririka mto mpya ambao utagawanyika na kuelekea Bahari ya Mediterania na Bahari ya Chumvi.
Na unapofika katika Bahari ya Chumvi, maji yake yatabadilika kutoka kuwa ya chumvi na kuwa safi, na kuleta matokeo ya kuwepo kwa samaki wengi wapya.
Na hekalu hilo litakuwa makao ya Kristo na serikali ya dunia
Yesu atatawala mataifa kutoka mahali hapa na serikali yake itaondoa uasi wote na tabia zote za dhambi hata miongoni mwa wale walio na dhambi
Taifa la Kiyahudi litatawaliwa na Daudi na mitume kumi na wawili, pamoja na taifa la Israeli lililotukuzwa
Na mataifa ya watu wasio Wayahudi (Wamataifa) yatatawaliwa na watakatifu wa kanisa waliotukuzwa, katika mfumo ambao haujulikani.
Na Isaya alisema wiki iliyopita kwamba tunapohitaji uongozi wa Yesu, tunaweza kumwita na Yeye hutujibu mara moja kutoka popote.
Sasa tunapoendelea na sehemu inayofuata, tunahitaji kuzingatia maisha ya kila siku, kuanzia na kwa nini serikali ipo wakati wa Ufalme.
Kimsingi, utawala ni mchakato wa kushughulika na wavunja sheria
Kama hakungekuwa na wavunja sheria, kusingekuwa na haja ya serikali
Kama Paulo anavyoelezea katika Warumi 13
Kusudi la serikali ni kuwa chombo cha Mungu ili kuhakikisha kwamba wavunja sheria wanaadhibiwa na tabia njema inahimizwa
Kwa hiyo, uhitaji wa serikali unatokana na athari ya dhambi.
Ukiondoa dhambi, tunaondoa pia hitaji la serikali ya aina yoyote, kwa sababu kila mtu angefanya yaliyo sahihi
Kwa hiyo, ukweli kwamba serikali ipo katika Ufalme ni uthibitisho (mwingine) kwamba dhambi ipo wakati huo
Na tulijadili awali katika somo hili jinsi baadhi ya watu watakavyoingia katika Ufalme wakiwa bado wamebeba dhambi pamoja nao.
Wameokolewa kwa imani yao, lakini wamekuja na mwili wenye dhambi kwani hawajawahi kufa.
Hebu tuchukue muda kurudia makundi mbalimbali ya wanadamu wanaoingia katika Ufalme.
Tulijifunza hapo awali kwamba kuna makundi matano tofauti ya waamini wanaoingia katika Ufalme Siku ya 1 huku wasioamini wote wakifa kabla ya hapo
Makundi matatu yanaingia huku wakiwa na miili mipya iliyotukuzwa, isiyo na dhambi, na watu hawa wa milele, wasio na dhambi, wanatawala pamoja na Yesu katika serikali.
Hawana dhambi, hivyo hawahitaji kutawaliwa wenyewe, na kwa sababu wanafanya mapenzi ya Yesu kikamilifu, wanaweza kusaidia katika kutawala.
Chini ya uongozi wa Kristo, wanahakikisha kwamba ulimwengu unatawaliwa kwa fimbo ya chuma katika haki kamilifu
Lakini makundi mengine mawili yanaingia katika miili ya asili, ya kidunia ambayo bado ina dhambi na hayatashiriki katika serikali.
Sharti la kuingia katika Ufalme halikuwa kutokuwa na dhambi, bali haki inayopatikana kwa imani
Kwa hiyo 100% ya wale watakaoingia katika Ufalme watakuwa waamini waliohesabiwa haki kwa imani, lakini si wote 100% watakuwa hawana dhambi.
Waamini hawa wenye dhambi wanaotoka katika Dhiki Kuu, Wayahudi na Mataifa, wataendelea kuishi katika miili ile ile waliyoingia nayo.
Hawajafa bado, kwa hiyo bado hawajafufuliwa katika miili mipya iliyotukuzwa
Na miili hii ya kawaida inaweza kuingia katika ndoa na kuzaa ili kuleta kizazi kipya cha wanadamu katika kipindi cha Ufalme.
Na vizazi vipya watakavyovizaa pia vitakuwa na miili ya kawaida, maana yake navyo vitakuwa na asili ya dhambi.
Lakini tofauti na wazazi wao, vizazi hivi vipya vya raia wa Ufalme (wale wanaoitwa “kizazi halisi cha Milenia”) si wote watakuwa waaminifu kama kizazi cha kwanza kilichoingia.
Kumbuka, hatuzaliwi tukiwa waamini…sote tunaingia duniani tukiwa tumeanguka na tunahitaji wokovu.
Ndiyo maana ni lazima tuzaliwe tena kwa imani wakati fulani katika maisha yetu ya kidunia
Kwa hiyo watoto wa Ufalme wataingia ulimwenguni wakiwa wenye dhambi na wasio na imani
Wale wote wanaoingia na dhambi watahitaji kutawaliwa, na hilo litakuwa kweli hasa kwa vizazi vijavyo vya wasioamini.
Watafanya makosa, na serikali itaingilia kati ili kuzuia makosa hayo yasienee
Hakuna dhambi itakayopata nafasi ya kukua au kusababisha madhara duniani kwa sababu itadhibitiwa haraka na kikamilifu.
Kwa hiyo kwa miaka 1,000 dunia itatawaliwa na kundi la wanadamu ambalo halifi, haliwezi kutenda dhambi na halitaoa au kuzaa.
Na wale tunaowatawala wataishi katika miili ya asili ambayo inaweza kufa, kuwa na dhambi na inaweza kuzaa watu wa asili wenye dhambi zaidi.
Na kadri muda unavyoendelea, watu hawa wa kawaida wataongezeka idadi na wataijaza tena dunia.
Lakini hali hiyo inafungua maswali ya kuvutia…maswali ambayo ni magumu kujibu katika baadhi ya matukio
Kwanza, maisha yakoje kwa wale waamini wanaoingia katika Ufalme?
Ni watu wangapi huzaliwa katika kipindi hiki? Je, wanakufa katika ulimwengu huu?
Na kama hawafi, tunawezaje kuwa na serikali isiyokua lakini inatawala idadi ya watu inayoongezeka bila kikomo?
Tukidhania kwamba ni watu 10,000 pekee, Wayahudi na Mataifa, wataokoka Dhiki na kuingia ulimwenguni wakiwa na miili ya asili.
Na kisha tuchukulie kwamba hao 10,000 ni takriban idadi sawa ya wanaume na wanawake na hao wote 10,000 wanaoa
Halafu tuchukulie kwamba asilimia 2 ya wanandoa hao wanapata mtoto mmoja kila mwaka, na kwamba hakuna mtu anayekufa,
Basi baada ya miaka 1,000, idadi ya watu duniani ingefikia trilioni 4!
Hilo linaonekana kuwa jambo lisilowezekana kulidhibiti. Kwa hiyo Biblia inatuambia nini kuhusu wakati huo?
Isaya anatupa maelezo haya kuhusu Ufalme
“Ushairi wa Isaya unatumia mistari miwili ya kishairi inayolingana (couplets) katika aya hii ili kueleza sheria za kifo katika Ufalme.
Katika mpangilio wa aya hii, mstari wa kwanza unaendana na wa tatu, na mstari wa pili unaendana na wa nne, hivyo kuunda jozi mbili za mawazo yanayolingana.
Hebu tuipange upya ili tuielewe kwa urahisi zaidi:
(1) Hakutakuwa tena na mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu,
(3) Kwa maana kijana atakufa akiwa na umri wa miaka mia moja
(2) Wala mzee ambaye hatatimiza siku zake;
(4) Na yule ambaye hatafikisha umri wa miaka mia moja atahesabiwa kuwa amelaaniwa.
Muhimu: Namba 4 inaeleweka vizuri kwa tafasiri ya karibu zaidi ya lugha ya awali. Kwa kutumia tafasiri ya "Swahili union version" inaweza ikakosewa kama haitazingatiwa kikamilifu.
Isaya anaripoti kwamba hakutakuwa tena na mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu
NNi wazi kwamba watoto watazaliwa katika Ufalme, jambo ambalo halitushangazi kwa kuwa tunajua kwamba watu wenye miili ya kawaida wataingia katika Ufalme.
Lakini mtoto hatakufa tena akiwa mchanga, jambo linalotulazimisha kukubali ukweli wa msingi: Mungu anadhibiti uhai na kifo
Mungu ametangaza kwamba katika Ufalme watoto hawatakufa wakiwa wadogo jambo ambalo linaweza kuwa kweli tu ikiwa Mungu atadhibiti wakati wa kifo.
Isaya anasema kwamba umri wa mapema zaidi ambao mtoto anaweza kufa ni miaka 100, na mtu huyo bado atachukuliwa kuwa kijana kwa sababu maisha yanaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi.
Bwana amemhakikishia kila mtu aliyezaliwa katika Ufalme angalau miaka 100 ya maisha
Ni wazi, hii ni tofauti kubwa sana na hali tunayoiona leo
Lakini kufa katika umri huo kutachukuliwa kuwa kifo cha mapema, Isaya anasema, jambo linalomaanisha kwamba muda wa kawaida wa maisha utarudi karibu na ule wa nyakati za Mwanzo.
Hata wanaume na wanawake wa kawaida wanaweza kuishi zaidi ya miaka 100 katika siku hizo
Kisha Isaya pia anasema kwamba mzee hatashindwa kuishi maisha yake yote katika Ufalme, ikimaanisha hatakufa kwa uzee pia.
Kwa hiyo watu wataishi mamia ya miaka, kama ilivyokuwa katika ulimwengu wa kale
Hatujui kwa uhakika kuhusu mchakato wa kuzeeka katika kipindi hicho, lakini inaonekana kwamba Mungu atawezesha miili ya kawaida kudumu kama ilivyokuwa hapo zamani.
Hii pia ni sehemu ya mageuzi au mabadiliko ya laana za Bustani.
Kabla Adamu hajatenda dhambi hakukuwa na kifo, lakini hata baada ya dhambi miili ilikufa polepole sana, kwani Adamu aliishi miaka 969.
Yule ambaye hatafikia mwaka wake (umri) wa 100 ataeleweka kuwa amelaaniwa
Kulaaniwa kunamaanisha kuanguka chini ya hukumu ya Mungu, ambayo katika muktadha huu inaonyesha hukumu ya milele katika Jehanamu
Tunajua kwamba wasioamini pekee ndio walio chini ya hukumu kutoka kwa Mungu, kwa hiyo wale waliolaaniwa lazima warejelee wasioamini katika Ufalme.
Hawa ni wazao wa waamini wa Mataifa waliozaliwa katika Ufalme katika miili ya asili
Watakufa wakiwa na umri wa miaka 100 na kuingia Jehanamu wakati huo
Kwa hiyo, kutimiza miaka 100 ya kuzaliwa kunaonekana kuwa hatua muhimu ya mabadiliko kwa wote waliozaliwa katika Ufalme
Ni wale tu wanaomwamini Yesu kama Bwana ndio watakaoruhusiwa kuishi zaidi ya miaka 100
Mara tu mtu anapoamini, anakuwa salama dhidi ya kifo kwa sababu Isaya anasema ataishi hadi mwisho wa Ufalme.
Kwa hiyo, ni hali ya kuchagua yote au kupoteza yote; asiyeamini ataishi miaka 100 tu, hatapewa zaidi ya miaka mia moja ya kuishi wakati waamini watafurahia maisha katika kipindi chote cha Ufalme.
Ni wazi kwamba huu ni utaratibu tofauti sana wa maisha na kifo ukilinganishwa na ule tunaoujua leo.
Na kwa njia hii Mungu anatuma ujumbe ulio wazi kabisa kwamba Ufalme unakusudiwa kufurahiwa na waamini
Na usahihi na ukali wa hukumu hii unaendana na mtindo wa jumla wa utawala wa Yesu: Anatawala kwa fimbo ya chuma
Ikiwa waamini hawafi katika Ufalme, basi ni lini wanapokea mwili mpya wa milele?
Na hii ni moja ya ukimya mkubwa wa Biblia…kwa sababu kwa ufahamu wangu hakuna Andiko linaloshughulikia swali hili
Ni wazi kwamba wakati fulani lazima wafufuliwe na kupewa mwili mpya wa milele usio na dhambi, kwa sababu tunajua kwamba baada ya Ufalme dhambi yote itaondolewa.
Lakini Biblia haituambii kamwe wakati ambao hili linatokea, kwa hiyo, tunalazimika kubashiri.
Huenda likatokea wanapofikisha miaka 100, au wakati wowote baada ya hapo, au mwishoni mwa Ufalme.
Wakati huo huo, hebu tuendelee kwenye swali linalofuata: mtu anawezaje kuishi miaka 100 duniani na Yesu akitawala Yerusalemu na asimwamini?
Wanafunzi wa Biblia mara nyingi hujiuliza inawezekanaje ulimwengu unaotawaliwa na Kristo kuwa na wasioamini.
Wengi hudhani kwamba Yesu ataonekana wazi kwa watu duniani
Na tunadhani kwamba maonyesho ya nguvu za kimiujiza yatakuwa ya kawaida
Hata ukweli kwamba sisi tutaishi miongoni mwa watu tukiwa na miili yetu ya utukufu ungeonekana kuwa ushahidi wa kutosha kuleta imani.
Lakini ukifikiria kwa kina zaidi, unakuja kugundua kuwa mambo haya hayawezi kuwa kweli katika Ufalme
Kwanza, kumbuka kwamba jambo hili tayari liliwahi kutokea wakati Yesu alipotembea duniani na kuonyesha nguvu na mamlaka yake.
Watu hawakumwamini wakati huo, kwa hiyo ni wazi kwamba inawezekana kumwona Mungu katikati yako na bado usishwishike kuamini
Pili, wasioamini katika Ufalme walizaliwa wakati wa Ufalme, kwa hiyo hawana uzoefu mwingine isipokuwa Ufalme.
Hawatajua chochote kuhusu kizazi kilichotangulia kabla yao, na hakutakuwa na ushahidi wa wazi wa enzi iliyopita.
Kama vile ulimwengu huu unavyokataa kuamini hadithi za Adamu na Nuhu, n.k. kwa sababu ushahidi wa kimwili unakosekana
Ndivyo itakavyokuwa wakati huo; watu watakosa ushahidi wa maisha yaliyokuwepo kabla ya Dhiki Kuu na kufanywa upya kwa dunia.
Tatu, hawatamwona Yesu kamwe katika kipindi chote cha miaka 1,000 ya Ufalme
Tutajifunza maelezo ya hekalu la Ufalme katika somo la wiki ijayo, lakini jambo moja tunalohitaji usiku wa leo ni makao ya Yesu.
Ezekieli 43 inatuambia kwamba Bwana anakaa katika Patakatifu pa Patakatifu ndani ya Hekalu kwa miaka 1,000 yote
"Bwana anarudi katika hali Yake ya kawaida ya utukufu, kama tulivyomwona Yohana akiieleza katika sura ya kwanza, na anakaa hekaluni bila kizuizi wala kukatizwa.
Na Ezekieli anaendelea kutuambia kwamba utukufu wa Bwana unaonekana tu kwa wageni wakati wa Sabato, sikukuu takatifu, na siku za mwezi mpya.
Na wasioamini hawaruhusiwi kamwe kuingia hekaluni au kuona utukufu wa Bwana…tutajifunza zaidi kuhusu hili wiki ijayo.
Kwa maneno mengine, yule aliyezaliwa katika enzi hii anaweza kuona kwamba hekalu lipo juu ya mlima mrefu huko Yerusalemu
Na mtu huyo pia ataona serikali ya watu wanaoutawala ulimwengu, lakini asiyeamini hatamwona kamwe Mfalme akiwa ameketi kwenye kiti Chake cha enzi ndani ya hekalu.
Kwa hiyo, njia pekee ambayo mtu asiyeamini atamtambua Yesu kama Mfalme ni kwa imani katika ushuhuda wa neno la Mungu.
Sharti la imani katika Ufalme ni kama ilivyo leo (na imekuwa hivyo siku zote)
Wokovu hauwezi kuwa jambo la kuona tu...lazima utokee kila wakati kutokana na imani katika neno la Mungu.
Biblia inafundisha kwamba imani ni udhihirisho wa tumaini, kwa sababu hukubali jambo kuwa kweli kabla halijaonekana kwa macho.
Mara tu kitu kinapoonekana, kukubali ukweli wake hakuhitaji tena imani…imekuwa dhahiri yenyewe
Wala kukubali ukweli huo hakupaswi kutupatia sifa yoyote, kwa sababu Mungu hapati utukufu wowote tunapotambua kile ambacho tayari ni wazi kabisa.
Kwa hiyo mpango wa Mungu wa wokovu unategemea imani, kuamini ahadi za Mungu zinazopatikana katika neno lake kuhusu mambo yajayo.
Tunaweka imani yetu katika vitu visivyoonekana, kifo cha Kristo kinachotupatia upatanisho, ufufuo na hukumu yetu ya baadaye
Neno la Mungu limetuahidi kuhusu mambo haya, na imani inahitajika ili kuyakubali
Sasa fikiria kama Yesu angeonekana katika umbo lake la utukufu kwa ulimwengu usioamini?
Bila shaka wangemkiri Yesu, lakini kukiri huko hakungekuwa kwa msingi wa imani katika neno la Mungu
Ingekuwa ukweli unaojidhihirisha, na kumtambua Yesu chini ya hali hizo hakungesababisha wokovu.
Hali hiyo si tofauti na ilivyo katika hukumu ya mwisho, kama Paulo asemavyo:
Katika hukumu ya mwisho, wanadamu wote kutoka historia yote wataelewa ukweli kwamba Yesu ni Bwana
Katika wakati huo, Paulo anasema kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri ukweli huo
Angalia kwa makini sehemu mbalimbali ambamo wanadamu watakuwa wakati watakapotoa ungamo hili.
Baadhi watakuwa juu ya dunia, wengine watakuwa duniani, lakini jambo la muhimu ni kwamba baadhi yao bado watakuwa chini ya dunia.
Na Paulo anasema kwamba hata wale walio chini ya dunia watamkiri Yesu, akimaanisha roho zilizo katika hukumu ya milele
Paulo anasema wao pia watamkiri Kristo kama Bwana, lakini watabaki katika hukumu licha ya kukiri kwao
Kwa nini? Kwa sababu wakati huo ungamo lao ni kukiri tu ukweli unaojidhihirisha ... hakuna imani inayohitajika
Na hivyo haileti wokovu
Hivyo, kwa kuwa kutoamini bado ni sehemu ya maisha katika Ufalme, basi imani lazima iendelee kuwa njia ya wokovu.
Na kama imani inahitajika, basi ukweli wa Kristo hautakuwa dhahiri kiasi cha kuondoa hitaji la imani.
Hiyo ndiyo sababu mojawapo inayofanya Yesu asiwe akitembea duniani katika mwili wake wa utukufu; badala yake, anabaki katika Patakatifu pa Patakatifu.
Ushuhuda wa siku hiyo utakuwa kwamba Bwana wetu anaishi hekaluni, akitawala na kuongoza
Lakini kukubali ushuhuda huo kutahitaji imani, kwa kuwa wasioamini hawatamwona Yesu wala hawataruhusiwa kuingia hekaluni.
Na kisha kuna suala la mwonekano wetu, na kwa sababu hiyo hiyo, tunapaswa kudhani kwamba mwonekano wetu mtukufu hautabadilika sana
Tunapaswa kutarajia kwamba muundo wetu wa mwili utafanana kwa kiasi kikubwa na huu tulionao sasa, ingawa bila dhambi, ugonjwa, au udhaifu.
Labda mwonekano wetu utabaki vile vile (bila makunyanzi na labda mwembamba kidogo).
Na ikiwa ni hivyo, hiyo inaweza kuwa njia ambayo tutatambuana
Na labda cha kushangaza zaidi, asili yetu isiyo na dhambi haitatufanya tuwe tofauti kabisa na wenye dhambi
Kumbuka, Yesu aliishi maisha yasiyo na dhambi, na bado hakuna hata mmoja wa ndugu zake wa kidunia aliyesukumwa na kile walichokiona kiasi cha kuamini madai Yake.
Kwa hiyo ikiwa Yesu asiye na dhambi angeweza kuishi pamoja na wasioamini bila wao kutambua, basi nasi tunapaswa kutarajia vivyo hivyo.
Tutaishi pamoja na wanaume na wanawake wa kawaida, lakini kutokuwa na dhambi kwetu hakutakuwa changamoto kwa kutokuamini kwao kwamba Yesu ni Mungu.
Hawatatuona na kushangazwa kiasi cha kumwamini Yesu mara moja.
Wanaweza kutuona kuwa watu wenye fadhili na wema, au kwa upande mwingine, wanaweza kuona kwamba wema wetu ni wa kiwango kisichowezekana kwa mwanadamu wa kawaida na hivyo kuhisi kushitakiwa dhamirani zao.
Hiyo ndiyo hali ninayojikuta nayo kila mara
Lakini jambo moja tunaloweza kujua kwa uhakika ni kwamba hali yetu ya kutokuwa na dhambi haitafuta hitaji la imani kwa wasioamini.
Kwa hiyo wasioamini siku hiyo watakaa na wale watakaowatawala bila kutambua tofauti iliyopo.
Wakati huo huo, sisi tuliotukuzwa tutafurahia siku zisizo na mwisho za furaha tukimtumikia Yesu na pengine tutakuwa na mahusiano mengi.
Tutaanzisha upya uhusiano na wale tuliowajua hapa duniani
Tutaanzisha uhusiano mpya na waamini kutoka kila kizazi, wakiwemo watu maarufu na wasiojulikana katika historia.
Mahali pengine katika Injili Yesu anatuambia tutashangazwa na wale wanaoingia katika Ufalme na wale wanaokosa kuingia.
Kutakuwa na watu katika Ufalme ambao waliishi maisha mabaya sana, lakini mwishoni walimwamini Kristo.
Na kutakuwa na watu watakaokosekana, ambao walikuwa na maisha ya uchaji Mungu na hata huduma maarufu lakini hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kweli na wa kibinafsi na Bwana.
Tutakuwa na miaka 1,000 ya kuzunguka dunia na kukutana na watakatifu wengi tuwezavyo na kujifunza hadithi zao.
Nadhani utalii siku hiyo hautakuwa wa kuona maeneo mengi bali utakuwa wa kukutana na watu zaidi.
Unaweza kusoma hadithi ya Yona siku moja na kuamua kumtafuta kwa ajili ya mazungumzo siku inayofuata.
Umewahi kujiuliza ilikuwaje kuwa ndani ya safina na wanyama kwa zaidi ya mwaka mmoja? Kunywa kahawa na Nuhu.
Unataka kujua kuvuka kwenye Bahari ya Shamu kulikuwaje? Zungumza na Musa au Miriam.
Unataka kumuuliza Haruni alikuwa anafikiria nini kuhusu yule ndama wa dhahabu? Unataka kumuuliza Ibrahimu alikuwa anawaza nini kuhusu Hagari? Basi jiunge na foleni ya wanaotaka kuuliza maswali hayo...
Kadiri tunavyofikiria mambo haya, ndivyo tunavyozidi kuwa na sababu za kutazamia maisha ya Ufalme.
Itakuwa kwamba kila kitu tunachopenda kwenye maisha ya leo kitakuwepo na bila kuwepo kitu ambacho hatupendi
Yatakuwa maisha yenye kuridhika na utimilifu badala ya kukatishwa tamaa
Yatakuwa maisha yenye maana badala ya maisha ambayo wakati mwingine yanaonekana hayana maana
Ni maisha yenye mpangilio na uthabiti unaoondoa hofu na wasiwasi
Maisha ambayo uzee na kifo vimeondolewa, na matokeo ya dhambi hayapo tena.
Siku zetu zitajaa kazi tunazozipenda, burudani zisizotudhuru sisi wala wengine, na mali zisizoharibika.
Na kwa asiyeamini, hali hiyo hiyo itakuwepo mradi tu hatendi dhambi na kama ataamini ndani ya miaka yake 100 ya kwanza.
Na katikati ya ulimwengu huo ulio karibu kuwa mkamilifu, asiyeamini ataambiwa lazima amwamini Yesu ikiwa anataka kuendelea katika furaha hiyo.
Ingawa tunaweza kudhani kwamba ulimwengu ulio bora kiasi hicho ungeifanya imani ipatikane kwa urahisi zaidi, ukweli utakuwa kinyume chake kabisa..
Wakati ulimwengu utakapokuwa na furaha kama hiyo, imani itakuwa ngumu zaidi
Kama ilivyo leo, watu wanapojikuta katika hali ya raha na utulivu, huwa na sababu chache sana za kutafakari kuhusu mabadiliko.
Hasa si mabadiliko makubwa kama ya kuacha njia yao ya sasa ya maisha na kutubu ili kumkubali Yesu na maisha mapya ndani yake.
Je, ni nini kingine tunachoweza kujua kuhusu maisha ya wakati huo? Hebu tuangalie kwa karibu maisha ya Kiyahudi katika Ufalme.
Kifungu hiki kinaanza na kauli inayojulikana, kwamba Israeli, tawi la Bwana, litakuwa zuri na nchi itatoa mazao mengi kwa ajili ya Israeli katika siku hiyo.
Na wote watakaosalia (baada ya Dhiki Kuu ) watakuwa watakatifu, kila mmoja aliyeandikwa kwa ajili ya uzima huko Yerusalemu.
Kama tulivyojifunza hapo awali, hakutakuwa na wasioamini katika Israeli
Kwa hiyo kutakuwa na Wayahudi wa kawaida, wasio katika hali ya utukufu, katika Ufalme (kama ilivyo kwa Mataifa).
Lakini tofauti na Mataifa, watoto wa Wayahudi wataonekana daima kuja kwenye imani katika Ufalme, au hivyo ndivyo inavyoonekana
Lakini pia tulijifunza hapo awali katika Ezekieli kwamba kutakuwa na vifo miongoni mwa familia za makuhani katika hekalu.
Kwa hiyo bado tuna fumbo kidogo kuhusu suala la maisha ya Kiyahudi
Isaya pia anasema kwamba Yerusalemu itafunikwa na utukufu wa Shekina wa Mungu kama kusanyiko la Israeli lilivyofunikwa jangwani wakati wa kutoka Misri.
Hekalu lenyewe ni sehemu ya mlima mkubwa unaojumuisha pia Yerusalemu na kufunika uwanda ule tuliouelezea hapo awali.
Uwanda tambarare ulioko juu ya mlima huu una ukubwa wa maili za mraba 50.
Mji wa Yerusalemu pia utakuwa huko juu, ukiwa na ukubwa wa maili 10 za mraba
Na kisha hekalu lenyewe ambalo lina ukubwa wa karibu maili moja ya mraba
Juu ya eneo hili lote kutakuwa na wingu wakati wa mchana ili kutoa kivuli cha kudumu na kulifanya eneo liwe baridi
Na usiku kutakuwa na moto unaowaka angani ili kutoa mwangaza wa kudumu juu ya hekalu
Na athari ya vyote viwili itakuwa kuzuia dhoruba au mvua kunyesha katika eneo hilo kama pazia la ulinzi.
Utukufu wa Bwana utaheshimiwa katika mambo haya
Vipi kuhusu maisha ya Mataifa katika Ufalme? Tunajua mambo machache tu kwa uhakika.
Katika Ufalme wageni, kwa maana ya Mataifa, watajiunga na Bwana ili kumtumikia kwa upendo wao kwake
Wataishi kama watumishi na watafuata sheria za kipindi cha Utawala wa Milenia, ambazo tutajifunza zaidi wiki ijayo.
Mataifa hawa wataletwa kwenye mlima mtakatifu na kuwa sehemu ya furaha ya nyumba ya sala
Tunajua kwamba "nyumba ya sala" ni neno la Agano la Kale linalorejelea hekalu lenyewe
Kwa hiyo Mataifa hawa watakuwa watumishi, na pengine hata makuhani katika Hekalu, na watatoa dhabihu mbele ya madhabahu kama makuhani.
Kwa njia hiyo hekalu litaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya watu wote
Katika wakati wa hekalu la zamani, ni Wayahudi pekee walioweza kutoa dhabihu, na hakika ni Wayahudi pekee walioweza kuhudumu kama makuhani.
Lakini katika Ufalme, hekalu litajulikana kama nyumba ya sala kwa watu wote, kwa sababu Mataifa watahudumu huko pia.
Na pia kutakuwa na maeneo mengine ya huduma kwa watu wa Mataifa katika Israeli katika kipindi hicho.
Katika Ufalme, Bwana atawajaza mataifa kote duniani kupitia Waamini Mataifa (Wamataifa waamini) wataoingia katika Ufalme siku ya kwanza.
Bwana anasema watazijua kazi Zake na kuuona utukufu Wake, kwa sababu kama tulivyosema awali, waamini wa Mataifa watapata nafasi ya kuingia Hekaluni.
Katika siku fulani za mwaka, wataweza kuingia na kushuhudia utukufu wa Bwana ndani ya hekalu.i
Na katika nchi wanazoishi, Bwana anasema pia ataweka ishara kati ya mataifa.
Ishara hiyo itakuwa ni wale waliosalia ambao Mungu atawatuma wakaishi huko—watakatifu wa Kanisa watakaokwenda kutawala huko
Sisi ni ishara kwa mataifa kwa ushuhuda wetu wa haki na imani tuliyo nayo.
Na Isaya anasema katika mstari wa 19 tutatangaza utukufu wa Bwana kwa mataifa hayo ya mbali.
Katika mstari wa 20 nabii anasema kwamba hawa watawarejesha ndugu wa Israeli Yerusalemu kwa farasi, magari ya vita na vitu na kadhalika.
Hii inaonekana kueleza siku za mwanzo za Ufalme ambapo Israeli inarejeshwa tena katika nchi yake.
Waamini wa Mataifa watawapeleka Wayahudi katika nchi yao kama ishara ya heshima na mabadiliko ya yale yaliyokuwa yametokea hapo awali ya kutawanyika.
Ambapo hapo kabla mataifa ya watu wa Mataifa haliisukuma Israeli kutoka katika nchi yake, sasa tunawarudisha kama vile kumtolea Bwana sadaka ya nafaka
Hatimaye, Isaya anathibitisha kwamba baadhi ya waamini hawa wa Mataifa watapewa heshima ya kuwa makuhani wanaohudumu hekaluni.
Hivyo waamini wa Mataifa watakuwa na nafasi ya uongozi katika serikali katika nchi za mbali ambako Bwana anatupatia urithi.
Lakini baadhi yetu tunaweza kuitwa kwenda juu zaidikwa wakuu ili kuhudumu ama kumtumikia Yesu Hekaluni.Yesu hekaluni.
Na baadhi ya watu wa Mataifa watapewa kazi ya kuhudumu moja kwa moja katika Israeli.
Isaya anasema kwamba wakati mataifa yatakapowaleta Wayahudi katika nchi mwanzoni mwa Ufalme, baadhi ya watu wa Mataifa hayo watabaki katika nchi hiyo.
Watafanywa kuwa milki ya Israeli kama sehemu ya urithi wa Israeli.
Na hao Mataifa watakuwa watumishi wa Israeli ingawa katika nafasi ya heshima
Nikisonga mbele, nilisema hapo awali kwamba dhambi haitapata nafasi ya kupata nguvu katika Ufalme, na hivyo maisha yatabaki ya amani katika wakati huo
Lakini kuna jambo la kuvutia ambalo ni tofauti na kanuni hiyo: ibada katika hekalu.
Sharti la mataifa ya watu wa Mataifa kutembelea hekalu mara kwa mara linaweza kupuuzwa
Na taifa linapokataa kutii sharti la kuja hekaluni, Bwana atalijibu kwa njia ya hukumu inayoweza kuleta maumivu au athari kubwa.
Mataifa yatahitajika kuja hekaluni kwa ajili ya sikukuu ya kila mwaka inayoitwa sikukuu ya Vibanda, ambayo ni sikukuu ya mwisho katika kalenda ya Kiyahudi.
Tutajifunza kuhusu sikukuu hii na matukio mengine ya ibada ya Ufalme wiki ijayo.
Jibu pekee ambalo Bwana ataleta kwa mataifa yanayokataa kufanya ibada hekaluni litakuwa ni ukame.
Kumbuka kwamba ardhi inatoa mazao kwa urahisi kwa sababu maji yanapatikana kwa wingi.
Kwa hiyo, mifumo ya umwagiliaji haitahitajika au haitajengwa, kwa kadiri tunavyodhania.
Kwa hiyo ukame utakuwa na athari ya haraka na kubwa sana kwenye kilimo na maisha, hivyo kuwa onyo au kizuizi chenye nguvu dhidi ya uasi.
Hatimaye, kwa Wayahudi na Wamataifa watakaokuwa wanaishi wakati huo, maisha yatakuwa ya kuridhisha na yenye kutosheleza.
Kwanza, tutajenga nyumba kwa ajili yetu wenyewe katika Ufalme, kama Isaya anavyosema.
Kama umewahi kutaka kubuni na kujenga nyumba hiyo nzuri kwa ajili yako mwenyewe, utapata nafasi hiyo
Na utaishi katika nyumba utakayoamua kujenga, na nadhani itakuwa nyumba inayozidi sana ile uliyonayo sasa.
Kwa kweli, kanuni ya jumla ya Maandiko ni kwamba maisha haya ni kivuli hafifu cha maisha tunayopata baadaye.
Ndiyo maana Biblia inatuonya dhidi ya kujiwekea akiba kubwa katika ulimwengu huu badala ya kusubiri thawabu yetu.
Na kama tulivyokwisha kujua, tutapanda mazao na kula matunda yake.
Hili ni zaidi ya kauli rahisi kuhusu kilimo… hoja ni uhakika wa kupata matokeo ya kazi yetu
Mimea haitakufa, mazao hayatashindwa kuota
Hakuna atakayevamia ardhi, hakuna atakayetunyang'anya nyumba yetu
Angalia katika mstari wa 22, Isaya anasema hatutajenga tunachokitaka halafu baadaye mtu mwingine akachukua kwa sababu yoyote.
Itakuwa yetu ya kudumu bila hofu ya kupoteza, kwa sababu Bwana ametupa kama urithi wetu
Vivyo hivyo, hakuna mtu mwingine atakayechukua mazao yetu kutoka mashambani
Na siku za maisha yetu katika wakati huu zitakuwa kama zile za mti, Isaya anasema
Kuna miti ambayo huishi zaidi ya miaka 2,000, na hivyo tutakuwa na maisha ya aina hiyo.
Kwa kweli, maisha yetu hayataisha kamwe, kwa hiyo kila siku itakuwa mwendelezo wa furaha yetu
Na tutafaidika na kazi ya mikono yetu.
Na kwa wale watakaooa na kuzaa, hawatafanya kazi bure, kwa sababu hakutakuwa na vifo vya watoto wachanga kama tulivyoona hapo awali.
Watoto wa wale waliobarikiwa na Bwana wataishi.
Na kila mzazi atapata furaha ya kulea watoto bila hofu ya kupoteza maisha yao
Baada ya kushughulikia yale tuliyoweza kupata kutoka katika Maandiko, bado kuna mambo mengi ambayo hayajashughulikiwa, bila shaka.
Hatujui kiwango cha teknolojia kitakachokuwepo katika Ufalme.
Je, kutakuwa na burudani, michezo? Je, tunaweza kuhamia sehemu mpya? Je, kutakuwa na fedha na uchumi?
Nafikiri Bwana amekusudia kuacha maswali mengi bila majibu ili maisha ya Ufalme yawe mfululizo wa mshangao usio na mwisho.
Na ninajikumbusha jinsi maisha haya ya sasa yanavyoweza kutushangaza na kutufurahisha licha ya hali mbaya ya dunia na watu.
Kwa hiyo fikiria jinsi itakavyokuwa bora zaidi wakati dhambi itakapodhibitiwa na na sisi tukiwa hatuna dhambi yoyote ya kibinafsi.
Na laana zimetoweka na dunia ina amani…nina uhakika hatutakosa enzi hii hata kidogo
Wiki ijayo tutaangalia shughuli za hekalu, ikiwa ni pamoja na kwa nini dhabihu hurejea
Na tunaangalia ibada katika Ufalme na kutembelea jengo la hekalu lenyewe kwa ufupi
Na kisha wiki inayofuata na ya mwisho ya Ufalme, tunaangalia matukio yanayohitimisha miaka 1,000