Taught by
Stephen Armstrong
Taught by
Stephen ArmstrongTumefikia somo la mwisho la mfululizo wetu wa kujifunza kitabu cha Ufunuo. Tunapofikia mwisho huu, tunakutana na sehemu ambayo huenda ndiyo yenye siri nyingi zaidi katika kitabu hiki na hata katika Biblia yote.
Yohana amepewa jukumu la kuelezea Mbingu Mpya na Nchi Mpya, na tunaweza kuelewa kwa urahisi jinsi kazi hiyo ilivyokuwa ngumu kwake.
Hatupi maelezo mengi kuhusu ulimwengu huo mpya, na yale machache anayoyatoa yanajikita zaidi katika mji mkuu wa ulimwengu huo, yaani Yerusalemu Mpya.
Katika somo la wiki iliyopita, Yohana alipewa utangulizi wa ulimwengu huu mpya kama mahali ambapo hakutakuwa tena na kilio, maumivu, machozi wala mauti.
Kwa maneno mengine, huko ndiko kutakakokuwa utimilifu kamili wa yote ambayo Mungu ametuahidi.
Ulimwengu huu haukuwahi kufunuliwa kwa watakatifu wa Agano la Kale… manabii waliokuwepo kabla ya Kristo (yaani waliotangulia Kristo) walipewa ufunuo kuhusu kipindi cha Ufalme pekee.
Lakini sasa Bwana anaanza kufungua pazia la kipindi hicho kitakachofuata katika historia, hata wakati sisi bado tunangoja kuja kwa Ufalme.
Kwa namna fulani, tunaweza kusema kwamba yale yatakayokuwa kweli kwa Israeli wakati wa Ufalme, hatimaye yatakuwa kweli kwa wanadamu wote katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Maono ya Yohana kuhusu ulimwengu huu mpya ni ya muda mfupi, lakini yanatoa maelezo ya kutosha kutuonyesha kwamba utakuwa tofauti kwa njia nyingi muhimu na ulimwengu wetu wa sasa.
Kama nilivyosema wiki iliyopita, tutaona tofauti kati ya ulimwengu wa sasa na Mbingu Mpya pamoja na Nchi Mpya ili kuelewa makusudi ya Mungu.
Kadiri tunavyoendelea na somo la leo, uelewa huo utaongezeka hatua kwa hatua hadi mwishoni, ambapo tutaona jinsi unavyoungana na kutoa picha kamili.
Ziara yetu inaanza na Yohana akiuona mji kwa mbali na kujiandaa kupima vipimo vyake na kuelezea uzuri na mpangilio wake.
Malaika aliyekuwa akimwongoza Yohana katika ziara hii anauelezea mji wa Yerusalemu Mpya kama Bibi-arusi wa Kristo.
Katika sehemu nyingine za Agano Jipya, jina “Bibi-arusi wa Kristo” hutumika kumaanisha watakatifu wa Kanisa.
Lakini tunapofika katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya, jina hilo linaonekana kuhamia na kutumika kwa mji wenyewe.
Hili linaeleweka vizuri tunapokumbuka kwamba neno “Bibi-arusi wa Kristo” linarejelea makao ya Roho wa Kristo.
Kama vile mume na mke wanavyokuwa mwili mmoja katika ndoa, ndivyo Yesu na Kanisa wanavyoungana kuwa mwili mmoja kupitia kukaa kwa Roho wake ndani yao.
Katika Enzi ya Kanisa, Bibi-arusi wa Kristo ni mwili wa Kristo, yaani Hekalu lake
Lakini katika enzi ya milele, Kristo anakaa pamoja na Baba katika Hekalu la mji, hivyo mji wenyewe unakuwa Bibi-arusi wa Kristo.
Na sisi pia tunaishi katika mji huo, hivyo nasi tutakuwa tukikaa pamoja na Kristo.
Mtazamo wa kwanza wa Yohana kuhusu mji huo ni wa kushangaza, ukianzia na umbo lake: ni mchemraba mkamilifu.
Urefu na upana wa jiji ni sawa na urefu wa majengo yake
Yohana hatoi maelezo ya kina kuhusu asili ya Nchi Mpya yenyewe ambako mji huo umejengwa, lakini anaona maono yake akiwa juu ya mlima mrefu.
Hivyo inaonekana kuna ardhi nje ya mji huo, ambayo baadaye Yohana ataielezea kwa kina zaidi.
Yohana anasema mji huo unang’aa kwa utukufu wa Mungu kama almasi, ikimaanisha utakuwa na mwangaza unaozidi hata mwanga wa jua la sasa.
Cha kushangaza, jiji limezungukwa na ukuta mrefu wenye malango matatu kila upande, hivyo kufanya jumla ya malango kumi na mawili.
Kwa kawaida, kuta hutumika kwa ulinzi, jambo linalotufanya tujiulize kwa nini mji huu unahitaji ulinzi?
Lakini baadaye katika mstari wa 25 tutajifunza kwamba malango hayo hayafungwi kamwe, hivyo ni wazi hakuna tishio la mashambulizi.
Kuta na malango haya si ngome za ulinzi, ni kumbukumbu za kukumbuka kazi ya Mungu katika Uumbaji uliopita.
Yohana anasema katika mstari wa 12-13 kwamba kila lango lilikuwa na malaika aliyesimama juu yake na kila lango liliitwa kwa moja ya makabila kumi na mawili ya Israeli.
Tunajua kwamba hatimaye Israeli ilikuwa na makabila kumi na matatu, kwa hiyo tunabaki kujiuliza ni majina gani kumi na mawili yanayotumika kwa malango haya
Makabila ya Manase na Efraimu huenda yamewakilishwa chini ya jina la Yusufu.
Milango ni sehemu ya kuingilia, kwa hiyo kuyataja malango kwa majina ya makabila kumi na mawili kunatukumbusha Israeli kuwa ni lango la ukombozi na la kumjua Mungu.
Mungu alifanya kazi kupitia Israeli ili kutimiza ahadi Zake za ukombozi kama Paulo alivyoelezea
Hivyo ni jambo linalofaa kwamba milango ya kuingia katika mji huo itakuwa kumbukumbu ya makabila kumi na mawili ya Israeli, kwa sababu bila Israeli hakuna mlango wa kuingia.
Bila Israeli, hakuna maagano, hakuna manabii, hakuna Sheria, hakuna hekalu, hakuna Kristo…kwa hiyo kweli kila mtu anaingia kupitia Israeli
Lakini kumbuka kwamba milango hiyo imepangwa kwa makundi ya mitatu, na hivyo kufanya jumla ya milango kumi na miwili, na namba hizi pia zina maana yake.
Namba tatu ni namba ya Uungu, ambayo inatukumbusha kwamba mbunifu aliye nyuma ya kila kitu ni Mungu.
Kazi yote ilikuwa ya Mungu pekee na bado aliikamilisha kupitia taifa la Israeli
Na namba kumi na mbili inawakilisha Mungu akitawala kupitia watu, hasa kupitia wana wa Yakobo.
Kwa hiyo malango yatatukumbusha milele kwamba Bwana alituleta katika mji huu kwa kufanya kazi kupitia familia inayoitwa Israeli.
Vivyo hivyo, Yohana anasema kwamba misingi ya mji huo itakuwa kumbukumbu ya jukumu la mitume.
Misingi ya kuta za mji itakuwa na tabaka kumi na mbili za vito vya thamani, kila moja ikiwakilisha mmoja wa wale mitume kumi na wawili walioteuliwa na Yesu.
Mitume hao ndio watu ambao Mungu aliwatumia kuanzisha Kanisa na kufungua njia kwa Mataifa kuingia katika mji huo pia.
Na ni jambo linalofaa kwamba mitume wawe kama misingi ya kuta hizo.
Kumbukumbu ya makundi haya mawili pamoja inasisitiza kwamba Israeli na Kanisa ni tofauti, lakini bado wanafanya kazi pamoja katika mpango wa Mungu.
Paulo anaelezea uhusiano huu katika Waefeso 2
Paulo anawaelezea Mataifa walio katika Kanisa kama warithi pamoja na Israeli katika nyumba ya Mungu.
Makundi hayo mawili yalitenganishwa na sheria ambayo Mungu aliwapa Israeli, lakini hakuwapa watu wa Mataifa.
Lakini sasa, kwa kuwa Kristo ametimiza kusudi la Sheria ya Musa, ameondoa ukuta uliokuwa ukiwatenganisha, na hivyo akawaruhusu wote wawili kuwa umoja.
Paulo anasema kwamba familia hii mpya iliyounganishwa imejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, yaani juu ya huduma yao ya kuleta na kutangaza ufunuo wa Mungu.
Kwa hiyo, katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya tutaishi katika mji uliojengwa kwa namna inayotukumbusha nafasi ya Israeli katika kufungua njia ya wanadamu wote kuingia katika neema ya Mungu.
Pia utatukumbusha nafasi ya mitume katika kupeleka Habari Njema kwa watu wa Mataifa.
Makundi haya mawili yanafanya kazi pamoja kwa utukufu wa Mungu, kwa kuwa aliwatumia wote kutimiza makusudi yake, jambo linaloonyeshwa pia na umuhimu wa namba kumi na mbili.
Sasa ziara yetu ya mji huo inaendelea, Yohana anapoanza kupima vipimo vyake na kueleza vifaa vilivyotumika katika ujenzi wake.
Kama tulivyoona katika maono ya hekalu katika kitabu cha Ezekieli, manabii walipewa vipimo vya majengo ili kuwapa wasomaji mtazamo sahihi na kuthibitisha uhalisia (ukweli) wa unabii huo.
Lakini zaidi ya yote, vipimo hivyo vinatuacha tukiwa na mshangao mkuu.
Yohana anasema katika mst. 16 kwamba mji huo umejengwa katika umbo la mraba makamilifu, ukiwa na maili 1,500 katika kila upande.
Ni wazi kwamba mji huo ni zaidi ya kitu chochote ambacho tumewahi kukiona duniani leo.
Mji wenye urefu wa maili 1,500 na upana wa maili 1,500 ungeenea karibu sehemu kubwa ya bara la Marekani
Na cha kushangaza zaidi, mji huo ni mchemraba, ukipanda juu kwa kimo kinacholingana na urefu na upana wake, yaani maili 1,500.
Katika sayari ya leo, sehemu kubwa ya nje ya angahewa ya Dunia ina kama maili 50 hivi tu.
Setelaiti huzunguka Dunia katika mizunguko iliyo kati ya maili 100 na maili 26,000 juu ya uso wa Dunia.
Kwa hiyo, mji huu ungefika katika eneo ambalo leo satelaiti huzunguka.
Hii inaonyesha wazi kwamba ulimwengu utakaoubeba mji huu utakuwa tofauti kabisa na dunia ya sasa.
Huenda angahewa yake itakuwa ya aina tofauti, au pengine katika uumbaji huo mpya haitahitajika tena kama ilivyo sasa.
Kuwa na ghorofa ya kifahari katika ulimwengu huu kunamaanisha kuwa na mandhari nzuri na ya kuvutia sana.
Vipimo katika mstari wa 15-17 pia vinasaidia kuimarisha maana fulani
Biblia yangu ya Kiingereza inatafsiri vipimo kama maili 1,500 kila upande huku ukuta ukiwa na urefu wa yadi 72.
Lakini vipimo vya awali vya Kigiriki viko katika dhiraa na stadioni
Kwa hiyo, maandiko yanasema mji una urefu wa stadia 12,000, na ukuta wake una dhiraa 144.
Vipimo hivi vya awali ni muhimu kwa sababumji wote umejengwa kwa mfumo unaozunguka namba 12 na vigawe (vizidishi) vya 12.
Tena, namba kumi na mbili ni namba ya utawala kamili wa Mungu kupitia wanadamu
Kwa hiyo mji huu ni ukumbusho wa mpango mkamilifu wa Mungu ambao aliutimiza katika Kristo kupitia Israeli na Kanisa.
Hatimaye, mji huo ni ushuhuda wa uzuri wa uumbaji wa Mungu katika fahari yake yote na utyukufu mwingi.
Kila mahali kuna vito kumi na viwili vya thamani, milango imetengenezwa kwa lulu imara iliyochongwa (yaani, milango ya lulu) na lami (njia) zake zimefunikwa kwa dhahabu safi.
Kitu tunachokithamini sana leo na tunachofanya kazi kwa bidii ili kukipata kitakuwa ni lami chini ya miguu yetu siku hiyo.
Kwa mara nyingine tena, matumizi ya mfumo wa namba kumi na mbili yanasisitiza uwezo wa Mungu wa kutimiza makusudi yake kupitia historia yote ya wanadamu.
Tunapoendelea na ziara yetu ya mji huo, Yohana sasa anaanza kuelezea wakazi wake, akianzia na wale wenye heshima ya pekee.
Yohana anasema kwamba hakutakuwa na hekalu katika mji huo, kwa sababu Mungu katika utimilifu wa Uungu wake ndiye hekalu la mji huo.
Hapo awali, Bwana alikaa pamoja na wanadamu kupitia jengo maalumu au ndani ya mwili wa mwanadamu, lakini katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya hakutakuwa tena na haja ya makao ya kimwili.
Mahekalu yalikuwepo hapo awali ili kumtenganisha mwanadamu na Mungu kwa sababu mwanadamu mwenye dhambi hangeweza kuwa mbele za Mungu mtakatifu.
Lakini dhambi yote itakapokuwa imeondolewa na maadui wote watakapokuwa wametoweka, Mungu katika utimilifu wa Uungu wake atakaa pamoja nasi katika uwepo wake mwenyewe. Kwa hiyo, yeye mwenyewe ndiye atakuwa hekalu.
Zaidi ya hayo, angalia kwamba Baba na Mwana wote wawili watakuwa wakikaa pamoja katika enzi hii, kwa kuwa hatimaye Baba ataweza kuwa na ushirika na mwanadamu tena.
Tangu wakati Adamu alipokuwa akitembea katika Bustani ya Edeni, jambo hilo halijawahi kuwezekana tena.
Na Paulo anatuambia katika 1 Wakorintho 15 kwamba Roho naye atakuwa akiishi katika hali hiyo pia.
Paulo anatuambia kwamba baada ya Ufalme, Mwana atamrudishia Baba mamlaka yote ili Mungu awe yote katika yote
Kifungu hicho cha maneno maana ya kina na yenye siri fulani, lakini yanaonekana kuashiria kwamba Mungu katika utimilifu wa Uungu wake atakuwa mwenye uwepo kamili, kama tunavyoona katika Yerusalemu Mpya.
Na kwa sababu Mungu atakuwa hapo kikamilifu, nuru ya ulimwengu huo mpya itatoka kwake mwenyewe.
Yohana anasema kwamba Mungu ndiye chanzo cha nuru, na hakutakuwa na jua wala mwezi wa kuangaza juu ya Nchi Mpya.
Utukufu wa Mungu wenyewe ni nuru kwa ulimwengu
Katika mstari wa 24 Yohana anaongeza kwamba mataifa katika ulimwengu huu hutembea kwa nuru ya Mwana-Kondoo
Inaonekana kwamba kutakuwa na mataifa duniani nje ya mji wa Yerusalemu.
Na tunasikia kwamba wafalme wa dunia huleta utukufu wao kwenye nuru lakini tunajua Paulo alisema kwamba mamlaka yote yamefutwa (yameondolewa)
Kwa hiyo msemo "wafalme huleta utukufu wao ndani yake" lazima iwe na maana kwamba wafalme wa dunia wanarejesha mamlaka yao
Ili utukufu wote sasa uwe kwa ajili ya Mungu na kutoka kwake
Hatimaye, katika mstari wa 25 Yohana anasema kwamba hakuna kipindi cha usiku katika ulimwengu mpya, jambo ambalo linatuletea maswali ya kuvutia.
Kwanza, linatufanya tujiulize kuhusu ujenzi wa ulimwengu mpya
Ikiwa Mungu ndiye mwanga pekee na Yeye anaishi katika mji huo, basi inaonyesha kwamba dunia ni tambarare
Kama dunia ingekuwa tufe, basi mwanga wa Mungu usingeweza kufikia upande wa nyuma wa sayari, na kusababisha giza huko
Au labda ulimwengu mzima una mwanga sawa au sheria za fizikia zimebadilishwa ... jibu halieleweki
Pili, tuna mambo mengi zaidi yanayoondolewa kutoka katika uzoefu wetu wa ulimwengu.
Awali tuliambiwa kwamba hakutakuwa na bahari katika ulimwengu huu mpya, na sasa tunaambiwa hakutakuwa na jua, mwezi, wala giza.
Kwa mara nyingine tena, hii inazua swali la kwa nini Bwana anabadilisha muundo?
Kwa nini alibuni ulimwengu wenye vipengele hivi mara ya kwanza ikiwa ulimwengu "ulio bora zaidi" hauhitaji hivyo?
Hebu tupitie simulizi ya Uumbaji…tukianzia na ukweli kwamba ulimwengu uliumbwa kutoka katika maji, kama Petro anavyotuambia
Petro anasema kwamba matumizi ya Mungu ya maji kama mwanzo wa uumbaji wa kimwili yalikuwa kielelezo cha mpango wake wa muda mrefu kwa dunia.
Mungu alijua kwamba siku ingekuja ambapo angeiangamiza dunia kwa maji, hivyo maji yalikuwepo tangu mwanzo wa uumbaji.
Zaidi ya hayo, uumbaji ulianza kwa kuwepo kwa nuru na giza tangu mwanzo, hata kabla sayari yenyewe haijakuwepo na kabla ya jua kuwepo.
Kwa hiyo, Bwana alikusudia kuwepo kwa vipindi vinavyobadilishana vya nuru na giza, na akaumba uumbaji unaolingana na mpango huo.
Mzunguko huu wa nuru na giza ulitoa ulifanya iwezekane kupima mwendo wa wakati. Kwa hiyo, wakati wenyewe uliumbwa katika Siku ya 1.
Na kuongezwa kwa jua na mwezi katika Siku ya 4 kulikuwa kwa ajili ya kutambua misimu (majira) na miaka
Katika muundo wa dunia ya kwanza, mchana na usiku viliwekwa ili kuonyesha mwendo wa wakati, na uwepo wa jua na mwezi ulitoa mpangilio wa vipindi katika mzunguko huo.
Kwa maana halisi, jua na mwezi havikuumbwa hasa ili kutoa mwanga, ingawa vilifanya kazi hiyo pia.
Mwanga ulikuwepo tayari katika Siku ya 1, na hivyo unaweza kuwepo tena bila jua kuuzalisha au mwezi kuuangaza kwa kuakisi mwanga wake.
Kusudi kuu la jua na mwezi lilikuwa kuwa ishara, kusaidia kuhesabu wakati na kuongoza majira ya dunia.
Lakini katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya hakutakuwa na haja ya kuhesabu wakati kwa namna hiyo (wala hakutakuwa na majira au ishara zitakazohitajika).
Sisi hufikiri juu ya wakati kama kitu kisicho na mwisho ambacho tunahesabu kwenda mbele ili kukumbuka umbali tuliotoka.
Lakini kwa mtazamo wa Mungu, wakati una mwisho. Kwa hiyo, kalenda yetu si hesabu inayopanda kwenda juu, bali ni hesabu inayoshuka kuelekea mwisho.
Ni hesabu ya kuelekea mwisho wa dunia hii na mwisho wa wakati wenyewe.
Na hivyo wakati hitaji la kuhesabu muda linapoisha, ndivyo vitu vilivyoumbwa kwa kusudi hilo pekee navyo vitakoma kuwa na umuhimu.
Bila usiku hakutakuwa na “siku” za kuhesabu, na bila jua hakutakuwa na “miaka” ya kuhesabu.
Hivyo, wakati katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya utakuwa wa milele yaani hauna mwisho, ingawa tutaona baadaye kwamba bado kutakuwa na kuhesabu miezi.
Sasa tunaingia katika sura ya mwisho, ambapo Yohana anatoa maelezo machache ya mwisho kuhusu ulimwengu huu mpya na wa ajabu unaokuja.
Sasa Yohana anaendelea kuelezea maelezo machache ya kuvutia kuhusu jiografia na vipengele vingine vya mji huo.
Kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu hutoka mto wa maji safi unaoitwa maji ya uzima unaotiririka katika mji.
Mto huo unapita katikati ya barabara pana ya mji na pande zote mbili za mto huo kuna mti wa uzima.
Kwa hiyo inaonekana kwamba mti huo umeenea pande zote mbili za mto, na unapata uhai (uzima) wake kutokana na maji hayo.
Kisha mti huo huzaa matunda kwa mpangilio wa kipekee wa kila mwezi, ukiwa na tunda tofauti kila mwezi.
Na majani yake yatakuwa na nguvu ya kuleta uponyaji kwa mataifa ya watu wanaoishi katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Mti huu ni mti wa pekee na wa kipekee unaoitwa Mti wa Uzima, na mara ya mwisho tunapouona mti huu ni katika Bustani ya Edeni kabla ya anguko la mwanadamu.
Cha kushangaza, Adamu na mwanamke walikula kutoka katika mti huu kabla ya kuharibiwa na dhambi, lakini walizuiwa kuufikia baada ya kutenda dhambi.
Mungu alisema kwamba hawangeweza tena kula kutoka katika mti huo, kwa sababu wangeishi milele.
Kwa hiyo, wakati Adamu na mwanamke hawakuwa na dhambi, walikula kutoka katika mti uliokuwa ukitoa uzima wa milele, lakini baada ya kuasi walizuiwa kuufikia tena mti huo.
Kwa kweli, kuwazuia Adamu na Mwanamke wasiingie kwenye mti wa uzima kulisababisha kifo cha kimwili kulingana na laana ya Mungu.
Walitoka katika mavumbi, na sasa bila kufikia mti wa uzima wangerudi mavumbini
Tunakumbuka kitu kama hicho kutoka katika maelezo ya hekalu linalopatikana katika Ufalme kama ilivyosimuliwa na Ezekieli na Zekaria.
Walielezea mto unaotoka hekaluni na kutoka nje ya jengo hilo ukigawanyika na kutiririka kuelekea mashariki na magharibi.
Katika maelezo ya Ezekieli, mto huo huleta uzima kila mahali unapopita, ikiwa ni pamoja na miti ya matunda ambayo majani yake yana uwezo wa kuleta uponyaji.
Kwa hiyo, kwa namna fulani, kufikia Mti wa Uzima ndiyo njia ya kupata uzima wa milele katika Ufalme na pia katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Hii inaelezea kwa nini mti huo pia ni sehemu ya mandhari katika Ufalme
Inaonekana kwamba kutokufa kimwili kunafanywa kuwezekana kupitia mti huo, katika Ufalme na katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Lakini kwa nini Mungu alianzisha utaratibu huu hapo mwanzo?
Angalia, kwamba mti wenyewe unategemezwa na maji yanayotoka katika kiti cha enzi, jambo linaloonyesha wazi kwamba uzima wote unatoka kwa Mungu.
Kwa hiyo, kila tunapokula kutoka katika mti huo au kutumia majani yake, tunakumbushwa kwamba uzima unatoka kwa Mungu na unatufikia kupitia mti huo.
Kwa namna hiyo, mti huo wenyewe ni chombo kinachotukumbusha chanzo cha uzima wetu.
Wakati mauti iko karibu kila wakati na afya ya mwanadamu ni dhaifu, tunakumbushwa daima kuhusu udhaifu wetu na utegemezi wetu kwa Mungu.
Lakini wasiwasi huo utakapokwisha, ni nini kitakachotufanya tukumbuke wema wa Mungu na nguvu yake ya kudumisha uhai?
Bila utaratibu kama huu wa mti wa uzima, tunaweza kuanza kuchukulia kutokufa kuwa jambo la kawaida na kusahau kwamba chanzo cha uzima wote ni Mungu..
Hatimaye, kumbuka kwamba mti huo huzaa matunda kwa mpangilio wa kila mwezi, na hii itakuwa njia ya kupima wakati katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Wakati utaendelea kupita na kupimwa, lakini utapimwa kwa miezi tu, si kwa miaka.
Kwa hiyo tunajua kila wakati ni mwezi gani, lakini hakuna mtu atakayehesabu miaka kwa sababu haitakuwa na umuhimu tena.
Hatutakuwa tukihesabu kuelekea jambo fulani linalokuja, na wakati wenyewe utakuwa wa milele kwetu.
Lakini bado tutakuwa tukifuatilia miezi katika mzunguko wa 12, huenda kwa ajili ya kusherehekea na kukumbuka matukio fulani yanayomhusu Kristo.
Jambo kuu litakuwa kumheshimu Mungu kupitia utaratibu huo wa ukumbusho.
Tukiendelea mbele katika kifungu hiki, katika mstari wa 3 Yohana anathibitisha kwamba laana aliyoitoa Mungu duniani baada ya dhambi ya Adamu kuondoka.
Katika Mwanzo 3 Mungu aliilaani ardhi kwa sababu ya Adamu, na kusababisha kifo cha kimwili na hatimaye kuharibiwa kwa Dunia hii.
Laana hiyo sasa imetimizwa, na kwa hiyo yenyewe imeondolewa.
Bila laana juu ya dunia, ulimwengu ungekuwa wa kupendeza kabisa na usio na dosari.
Muhimu zaidi, hatutakuwa tena chini ya hukumu wala hatutashughulika na athari za dhambi katika dunia yenyewe.
Hakutakuwa na magugu, hakutakuwa na kazi ngumu yenye uchungu, na zaidi ya yote hakutakuwa na dhambi wala mauti.
Kazi tutakayofanya itakuwa katika kumtumikia Kristo. Hatuwezi kusema kwa hakika itakuwaje, lakini tunajua itakuwa kazi yenye thamani na yenye furaha.
Ukamilifu wetu unamaanisha tutafanya kazi katika uwepo Wake na kuuona uso Wake
Naye atatutambulisha kuwa wake kwa kuweka jina lake juu yetu, muhuri unaotuhakikishia kwamba hatutakabili tena mauti wala dhambi milele.
Mwishowe katika mstari wa 5 Yohana anarudia kusema kwamba hakuna usiku, na hakuna haja ya taa wala jua, kwa sababu nuru ya Mungu itakuwa kila mahali.
Hakutakuwa na giza popote, hata kivuli hakitakuwepo.
Hakutakuwa na kitu kama chumba chenye giza au kabati lenye giza… nuru itakuwepo kila mahali bila kukoma.
Pia tunaweza kudhani kwamba hatutakuwa na haja ya kulala tena.
Kabla hatujamaliza sura hii, hebu tufanye mapitio hayo ya tofauti zote kati ya uumbaji wa kwanza na uumbaji huu mpya.
Tunapoweka tofauti za uumbaji huu miwili pamoja, tunaona muundo fulani.
Uumbaji wa kwanza ungekuja kuharibiwa na dhambi katika Bustani ya Edeni, na kusababisha laana juu ya dunia na hukumu.
Kwa hiyo, katika Uumbaji wa awali, Bwana alijumuisha vipengele fulani katika muundo wa dunia kwa kutarajia kuja kwa dhambi.
Vipengele hivi vingekuwa muhimu kwa Mungu katika kumwonyesha mwanadamu kweli muhimu za kiroho kuhusu dhambi na ukombozi.
Kwa mfano, Bwana aliumba ulimwengu wenye nuru na giza ili aweze kutumia maneno haya kuelezea haki na dhambi.
Na Bwana aliumba bahari akijua angeitumia kuiangamiza dunia wakati dhambi ilipoenea sana katika siku za Nuhu.
Zaidi ya hayo, katika Maandiko, kina cha maji mengi kinachofunia dunia hutumiwa kama taswira ya Sheol, yaani makao ya wafu.
Neno la Kiebrania linalotafsiriwa “kilindi” ni tehom, nalo ndilo neno linalotumiwa pia katika sehemu nyingine za Maandiko kumaanisha vilindi vya bahari.
Kwa hiyo Bwana aliumba ulimwengu wenye usiku na bahari ili kumruhusu kuonyesha dhambi na kifo na adhabu ya milele.
Na Bwana alijumuisha vitu kama jua na mwezi ili kuanzisha kuhesabu muda na kutoa ishara za mwisho.
Kuhesabu muda kulihitajika ili kuwapa watu nafasi ya kuashiria utimilifu wa unabii kuhusu mwisho wa enzi
Pia, jua na mwezi vinatumiwa na Mungu kama ishara za mwisho wa enzi hii unaokaribia na hukumu inayokuja dhidi ya dhambi.
Zaidi ya yote, kumbuka kwamba Bwana alifanya maamuzi haya ya usanifu (muundo) kwa ajili ya dunia ya kwanza muda mrefu kabla ya mwanadamu kuwepo au kabla ya Adamu kuanguka katika dhambi.
Kwa maneno mengine, mpango wa Mungu kwa uumbaji wa kwanza tayari ulikuwa umezingatia kuja kwa dhambi, na muundo wa uumbaji huo uliandaliwa ili kuendana na hali hiyo.
Bwana alipanga kutumia mambo haya kufundisha maana yake ya kiroho na kufunua mpango wake wa kuyaondoa kupitia Mwana wake, Yesu Kristo.
Lakini sasa, kwa kuwa hakuna tena kitu kilicho najisi katika ulimwengu wote, hakuna anayefanya dhambi, na mauti haipo tena, vipengele hivyo havina tena sababu ya kuwapo.
Mbingu Mpya na Nchi Mpya zimeumbwa bila vielelezo hivyo, kwa sababu mambo ambayo vilikuwa vinayawakilisha hayapo tena.
Sasa kwa kuwa dhambi imeondolewa na haitarudi tena kamwe, Mungu ameumba ulimwengu tofauti, unaofaa kwa kusudi jipya.
Ingawa ulimwengu wa kwanza ulikuwa makao ya mwanadamu aliyeanguka katika dhambi, ulimwengu mpya ni makao yaliyokusudiwa kwa mwanadamu aliyetukuzwa na asiye na dhambi.
Mpango wa Mungu kwa uumbaji tangu mwanzo ulijumuisha kuruhusu kuingia kwa dhambi, ili hatimaye Kristo aje katika uumbaji huo na kufa kwa ajili ya kuukomboa.
Ingawa Mungu si chanzo cha dhambi, alijua kwamba dhambi ingeingia duniani na akaweka mpango wa kushughulikia hali hiyo.
Kwa sababu uumbaji ulipaswa kujua dhambi ni nini na kuelewa hukumu ambayo dhambi inastahili, ili uweze kufahamu kikamilifu kina cha upendo wa Mungu.
Ni lazima tuelewe kwamba Mungu ni Mungu wa ghadhabu dhidi ya dhambi na wa hukumu ya haki, ndipo tutakapoweza kumsifu kwa neema na rehema zake.
Na sasa, katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya, tutamkumbuka na kumtukuza Mungu milele kwa mpango wake wa ukombozi alioutekeleza kwa ajili yetu.
Kwa kuelewa hayo, tunaingia katika maneno ya mwisho ya Kristo aliyomwambia Yohana na sisi pia.
Kristo anamalizia maono ya kitabu hiki kwa namna ya kibinafsi kwa Yohana, akianza kwa kusema kwamba maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli.
Tunaweza kuamini rekodi ya kitabu hiki na kuipokea kwa ujasiri kamili kwamba haya ndiyo yatakayokuja kutokea, na kwamba wakati huo hauko mbali.
Roho yule yule aliyewapa manabii maneno yao ndiye aliyempa Yohana maneno haya.
Soma Isaya na uone mambo yote yaliyoandikwa zamani kuhusu Yesu ambayo yalitimia
Soma Danieli na uangalie matukio yote ya ulimwengu yaliyotokea kama vile Danieli alivyosema
Je, watu hao walibahatisha tu? Haiwezekani! Walijua wakati ujao kwa sababu Mungu aliwafunulia
Na Yohana yuko katika hali ile ile…aliona mambo yanayowakilisha mustakabali wako, na mambo hayo yana uhakika kama neno la manabii
Yesu anasema kwamba anatuonyesha sisi watumwa wake, mambo ambayo lazima yatokee hivi karibuni
Lakini tunajua maneno haya yaliandikwa miaka 2,000 iliyopita…je, hayo yako karibu vipi?
Kwa sababu yatakapoanza kutimia, yatatokea kwa haraka, na kwa mtazamo wa umilele kipindi hicho kitakuwa kifupi sana.
Kwa hiyo tunapaswa kufanya nini wakati tunangoja? Yesu anajibu hilo katika mstari wa 7 akisema, kumbuka kwamba anakuja upesi, ambayo ni rejea ya Unyakuo
Kwa kuzingatia mambo yatakayotokea, Yesu anasema tunapaswa kuishi tukiwa tunafikiria mwisho kila wakati.
Tunapaswa kuishi tukiwa na macho ama mtazamo wa umilele, tayari kwa kurudi kwa Bwana.
Na kuyashika maneno ya kitabu hiki kunamaanisha kuruhusu ukweli wa mambo haya yajayo kuathiri maamuzi tunayofanya katika maisha.
Ni jambo moja kukubali kiakili (kwa ufahamu wa akili) kwamba siku moja mambo haya yatatokea.
Lakini ni jambo lingine kuruhusu maarifa hayo kubadilisha namna tunavyoishi.
Ili kusisitiza zaidi umuhimu wa jinsi tunavyopaswa kuitikia, Yohana anaeleza katika mstari wa 8 kwamba alianguka chini na kutaka kumwabudu malaika aliyekuwa akiongozana naye.
Lakini Yohana anakemewa na malaika huyo na kukumbushwa kwamba hatupaswi kuwaabudu watumishi wenzetu wa Mungu.
Hilo liwe ukumbusho kwetu kwamba tusimwinue mtumishi yeyote wa Mungu, awe mwanadamu au kiumbe wa rohoni, zaidi ya kiwango kinachofaa.
Kisha katika mstari wa 10 Yohana anaambiwa kwamba tofauti na mtangulizi wake, Danieli, yeye hapaswi kuuficha unabii huo kwa kuufunga muhuri…anaambiwa anapaswa kuuacha wazi
Kumbuka, Danieli aliambiwa afunge maono yake kwa sababu hayangefunuliwa kikamilifu hadi siku za Yohana, jambo tulilojifunza katika sura ya 11.
Unabii aliopewa Danieli ulikuwa umetabiriwa mapema sana kiasi kwamba haungeweza kuwa na manufaa kwa watu wa wakati wake.
Lakini sasa wakati umekaribia, hivyo ulimwengu unahitaji kusikia na kuelewa maana ya kitabu cha Ufunuo.
Hiki si kitabu cha kuogopa au kukiepuka. Kinyume chake, kitabu chenyewe kinatangaza baraka kwa wale wanaokisoma na kujifunza kutoka kwake.
Sasa malaika anamwambia Yohana kwamba wakati umekaribia, na tunahitaji kuelewa maana ya kitabu hiki.
Kwa kweli, maana ya kitabu hiki itakuwa wazi zaidi kwetu tunapokaribia mwisho
Hiyo ni sababu mojawapo inayonifanya niamini kwamba tuko karibu sana, kwa sababu maana ya kitabu hiki imekuwa wazi zaidi kwetu.
Kwa upande mwingine, katika mst. 11 Yohana anakumbushwa kwamba ukweli kwamba kitabu hiki kinaweza kueleweka katika wakati wetu haimaanishi kwamba wasioamini watafaidika nacho.
Kinyume chake, malaika anasema wasioamini wataendelea kufuata njia zao za dhambi
Ni pale tu Roho atakapokatiza mwelekeo huo kwa kuwapa imani ya wokovu ndipo hali hiyo itabadilika.
Wakati huo huo, wale walio na kweli wataendelea kuwa katika mkono wa Kristo hadi mwisho.
Kisha katika mstari wa 12-15 Yesu mwenyewe anatoa wito wa mwisho kwa mwamini na kwa asiyeamini.
Lichukulie hili kama mwito mkuu wa mwisho wa Biblia wa kuitikia wito wa Mungu, nafasi ya mwisho kwa msomaji kutafakari juu ya yote ambayo Biblia imeyashuhudia.
Kwa mwamini, Yesu anasema kwamba anakuja upesi, yaani bila onyo, na anakuja na thawabu yake.
Atatulipa kwa matendo yetu tuliyoyafanya kwa kumtumikia Yeye
Na katika mst.14 Yesu anazungumza na wasioamini akiwaalika kutamani mema yaliyoelezwa katika kitabu hiki.
Kusafishwa dhambi zao kwa damu ya Yesu, kula matunda ya mti wa Uzima badala ya kuangamia katika Ziwa la Moto, na kuingia kupitia milango ya mji.
Yesu anawakumbusha wale wanaokataa wito wake katika mstari wa 15 kwamba hao ni wale wanaoendelea kupenda na kutenda mambo yasiyo ya haki ya dhambi.
Kumbuka kwamba Yesu hasemi kwamba kila anayefanya mambo haya moja kwa moja hana wokovu.
Anasema kwamba tabia hizi zinaonyesha mtindo wa maisha na mtazamo wa wasioamini
Na ikiwa wale wanaoishi katika mambo hayo hawatatubu na kuamini, wataachwa “nje” ya mji.
Tunajua kwamba wasioamini wataendelea kuwepo milele katika Ziwa la Moto, na sasa tunapata wazo ama dokezo kuhusu mahali ambapo huenda panaweza kuwa.
Kwa kuwa Mbingu na Nchi za kwanza zimepita, Ziwa la Moto lazima liwe limepewa nafasi (mahali) katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Na mahali hapo papya ni mahali fulani nje ya mji
Hili linaacha uwezekano kwamba eneo hilo linaweza kuonekana kutoka katika mji, au angalau likawa bado liko mahali fulani duniani.
Hatimaye, kitabu chetu kinaisha kwa baraka ya mwisho…
Yesu anashuhudia kwa mara nyingine ya mwisho kwamba tunapaswa kutumaini na kuamini yale aliyotupatia, na kumtumaini yeye kama Masihi, mzao wa Daudi.
Mwisho wa kitabu hiki unatupa hisia kwamba Yesu alijua kitabu hiki kingetiliwa shaka, kingepingwa, kingeelezewa vibaya, na hata kingepuuzwa na baadhi ya watu.
Lakini hakuna kitabu kingine cha Maandiko ambacho Yesu anazungumza moja kwa moja na msomaji kwa nafsi ya kwanza kama Kristo aliyefanyika mwili (aliyekuja katika mwili).
Na hakuna kitabu kingine cha Maandiko ambapo Yesu anasisitiza kwa nguvu sana kwamba neno linapaswa kuaminiwa na kufuatwa.
Na kisha Yesu anatoa wito mmoja wa mwisho kabisa wa kuitikia wito wa Mungu, wito wa mwisho wa kuamini ujumbe wa Biblia yote
Katika mstari wa 17, Roho na Kanisa wanauambia ulimwengu, “Njoo,” wakimaanisha njoo kwenye imani katika Yesu.
Tangu karne ya kwanza, Roho wa Mungu na Kanisa la waamini wamekuwa wakiuita ulimwengu kumjua Yesu.
Na yeyote anayekuja akiwa na kiu ya haki na amani atapokea maji ya uzima bure.
Lakini kinyume kabisa na mwaliko huo, kitabu kinaishia na onyo linalopaswa kumfanya kila mtu afikirie kwa makini kabla ya kubadilisha au kupotosha Maandiko.
Yesu anasema kwamba yeyote atakayefanya mabadiliko katika kitabu hiki, hataingia katika mji wa Mungu.
Atapata mapigo yote yaliyoelezwa katika kitabu hiki, ambayo hatimaye yanaishia katika Ziwa la Moto.
Huenda wasipitie au waisiishi katika kipindi cha Dhiki Kuu, lakini jambo kuu ni kwamba watapata mateso moja au zaidi yanayozungumziwa katika kitabu hiki.
Jambo la hakika ni kwamba, watakabili Ziwa la Moto.
Yesu anasema kwamba tamaa ya kudhoofisha Neno la Mungu ni sifa inayodhihirisha kutokuamini.
Kubadilisha neno la Mungu ni ishara ya uhakika kwamba mtu huyo hana uhusiano wowote na Roho aliyeandika neno hilo.
Ndiyo maana Yesu anasema kwamba hawatapatikana katika Kitabu cha Uzima.
Lugha ya mstari wa 19 inaweza kusikika kana kwamba Yesu anasema mtu anaweza kupoteza wokovu.
Lakini hiyo ni matokeo tu ya Yesu kutumia lugha yenye usambamba wa makusudi. Anasema: “Ukiondoa maneno yangu, mimi nakuondoa wewe”
Na kwa kuwa Roho ndiye mwandishi wa Biblia yote kama kazi moja iliyoungana, basi kwa mantiki hiyo onyo hili linatumika kwa vitabu vyote vya Biblia.
Kazi yote ya Maandiko ilivuviwa na Mungu, ikijumuisha pia idadi maalumu ya vitabu vilivyomo katika orodha rasmi ya Maandiko matakatifu.
Kwa hiyo Mungu alijua maneno haya yangekuwa maneno ya mwisho ya Biblia
Hilo linaonyesha wazi kwamba onyo lake lilikuwa dhidi ya kubadilisha chochote katika Neno la Mungu lote, si katika kitabu cha Ufunuo pekee.
Hatimaye, Yesu anatuhakikishia kwamba anakuja upesi, jambo ambalo Yohana anaongeza, Amina, njoo Bwana Yesu
Nami pia nasema, Amina.
Neema ya Bwana Yesu iwe nasi sote…hata atakapokuja
Tafadhali jifunze mambo haya, na yashirikisheni kwa wengine.